Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara imewezesha kupatikana na hatimaye kulipwa wafanyakazi vibarua 27 jumla ya shilingi milioni 17,737,887 walizokuwa wanamdai, Bw. Thomas Meliyo Rikoyan mkulima mkubwa wilayani Simanjiro, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, Adam Kilongozi ameyabainisha hayo leo Oktoba 19, 2020.
Bw. Thomas Meliyo Rikoyan mwenye mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya ekari elfu mbili wilayani Simanjiro ameajiri kwa kuwaweka kambini kwake vibarua 27, kazi yao ikiwa ni kulima, kupanda, kupalilia, kuvuna, kupukuchua (mahidi) na kupigapiga maharage.
"Mnamo Oktoba 9, 2020 TAKUKURU Mkoa wa Manyara ilipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya vibarua hao wakimlalamikia Bw.Thomas Meliyo Rikoyan kwamba tangu mwezi Novemba,2019 hadi sasa wamekuwa wakifaya kazi kwenye masdhamba yake bila kulipwa mshahara kinyume na makubaliano ya mikataba ya ajira zao.