Kampuni ya TMS Consultants imewataka vijana 200 wa vyuo vikuu ambao wamemaliza Shahada ya Kwanza na wanategemea kuendelea na kozi yoyote ile kuhudhuria katika uzinduzi wa programu maluum unaotarajiwa kufanyika kesho Oktoba 3, mwaka huu katika Hoteli ya Peacock iliyopo Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Sebastian Kingu, amesema kuwa program hiyo imelenga kuwasaidia vijana kupunguza tatizo la ajira jambo ambalo limekuwa ni kilio kikubwa nchini Tanzania.
"Tumekusudia kuwasaidia vijana ambao hawapo katika ajira rasmi kwa kushirikiana na washirika wa kimkakati wakiwemo Enterprise Finance (EFL),Madson Property Co.Ltd, Salvation Farm and Marketing Co Ltd,Agricom Africa Ltd pamoja You spices and Green Integration Co.Ltd,"amesema Kingu.
Amesema kuwa, kila mwaka vijana laki nane Tanzania huingia kwenye soko la ajira ambapo hii hujumuisha wote waliomaliza vyuo na wale walio katika vyuo vya ufundi na ujuzi mbalimbali kwani asilimia tano ndio ambao huingia katika ajira rasmi sawa na vijana 40000 kila mwaka.
Ameongeza kuwa, vijana 760,000 sawa na asilimia 95 huingia kwenye kudi la wasio na ajira rasmi hali inayopelekea wengi wao kuingia katika sekta zisizo rasmi na kusababisha kufanya kazi ambazo hazina tija katika mustakabali wa maisha yao.