TTB, CLOUDS MEDIA GROUP NA SHIRIKA LA NDEGE LA PRECISION KUSHIRIKIANA KUTAGAZA UTALII WA NDANI

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesaini mkataba wamakubaliano na kampuni ya Clouds media group pamoja na Shirika la ndege la Precision Air kwa lengo la kuungana pamoja katika kuwahamasisha Watanzania kufanya utalii wa ndani kupitia kampeni ya “Twende Serengeti” inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe 16 Oktoba 2020,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kampeni ya Twende Serengeti imeandaliwa hususani kwa ajili ya watanzania kwenda kuembelea hifadhi ya Serengeti ili kujionea msafara wa nyumbu wanaohama kutoka Tanzania na kwenda nchini Kenya na kurudi tena Tanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB, Jaji Thomas Mihayo (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Precision Air, Patrick Mwanri wakiwashuhudia Mindi Kasiga (kulia), Mkurugenzi wa Masoko wa TTB na Lilian Massawe wakisaini mkataba wa maelewano katika hafla iliyofanyika katika ofisi za TTB jijini Dar es Salaam.
Akiongea wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Bi.Mindi Kasiga amesema ,“Kampeni ya Twende Serengeti ni moja ya mkakati wa TTB katika kuwafanya Watanzania kujenga utamaduni wa kuvitembelea vivutio vya utalii vya Tanzania. 

Aidha, Bi. Kasiga ameongezea kuwa, TTB ipo bega kwa bega na wadau wa sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya habari na sekta ya usafiri na hilo linadhihirishwa na tukio la leo Oktoba 9,2020 la uwekaji saini wa mkataba huu wa makubaliano wa miaka mitatu na Clouds Media Group ambao tutatumia chombo hicho katika kuitangaza kampeni hiyo.

Bi.Mindi ameeleza kuwa, kwa upande wa usafiri, "tumesaini mkataba wa makubaliano na shirika la ndege la Precision Air ambalo limetoa ndege mbili kwa punguzo maalum zenye uwezo wa kubaba abiria 48 kutoka Dar es Salaam mpaka Serengeti na kurudi Dar es salaam ambapo watalii wataondoka Dar es Salaam Oktoba 16 na kurudi Oktoba 18,"amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB, Jaji Thomas Mihayo (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga wakiwashuhudia Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Mindi Kasiga (kulia) na Sheba Kussaga, Mkurugenzi wa Biashara na Mendeleo Clouds Media Group wakiweka saini mkataba wa malewano wa miaka mitatu.
Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Bw. Joseph Kusaga ametumia nafasi hiyo kuishukuru TTB kwa kushirikisha wadau wa vyombo vya habari katika kampeni hii ambayo itasaidia kuongeza idadi ya watalii wandani.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Precision Air, Patrick Mwanri amesema kwa kushiriki katika kampeni hii itazidi kujenga imani kwa wateja wa ndani na nje ya Tanzania wa shirika hilo la ndege na kuvutia wengi kutumia huduma ya shirika hilo.
Mwanasheria wa TTB, Irene Mugyanyizi (Kushoto) akigonga mhuri katika moja ya mikataba iliyosainiwa na pande zote mbili Mindi kasiga (kulia), kuhalalisha makubaliano hayo kisheria.
"Bodi ya Utalii Tanzania itaendelea kufanya kampeni za kuwapeleka watalii wa ndani katika maeneo mengine ya vivutio vya utalii na kuwakaribisha wadau wengine kuunga mkono kwa kushirikiana na TTB katika kampeni zinasofuata. Utalii wa Tanzania unaanza na Mtanzania mwenyewe,"amesema Bi.Mindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news