Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania wote wakiwemo na wakazi wa wilaya ya Karatu ifikapo Oktoba 28 mwaka huu wajitokeze kwa wingi kwenda kumchagua Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM kwa sababu ni kiongozi sahihi, anaripoti Sophia Fundi, Karatu.
“Dkt. Magufuli ni kiongozi sahihi, atakayeweza kuratibu maliasili zetu na kuzikusanya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Mnajua tulivyokuwa tunaibiwa katika madini lakini leo hakuna anayetuibia ni kwa sababu ya kuwa na kiongozi muadilifu anayeweza kuongoza na kuwatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.”
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Oktoba 16, 2020 alipozungumza na wakazi wa wilaya ya Karatu kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Mazingirabora wakati akimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Karatu, Daniel Awack na wagombea udiwani wa CCM.
“CCM ndio chama pekee kitakachowaletea maendeleo na hamtojuta kuwachagua viongozi wa CCM. Mambo yote ya maendeleo Karatu yapo ndani ya Ilani. Kitabu cha Ilani kimejaa miongozo na maelekezo ya kuwatelea maendeleo Watanzania wote. Tumpe Dkt. Magufuli ridhaa ya kuongoza miaka mitano mingine ili atuletee maendeleo.”
Amesema, wananchi wanatakiwa wamchague Dkt. Magufuli ili andelee kuwaletea maendeleo kwa sababu katika kipindi cha miaka mitano ya awali ameweza kuwaletea mabadiliko makubwa katika huduma mbalimbali za jamii zikiwemo za afya, elimu, maji na miundombinu. Amewaasa wasikubali kudanganyika wamchague Dkt. Magufuli.
Akizungumzia kuhusu usambazaji wa nishati ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa amesema zaidi ya vijiji 9,300 nchini vimefikishiwa umeme kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015, hivyo hali ya upatikanaji wa umeme imeimarika, watumiaji wa umeme wameongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 hivi sasa.
Hivyo, amewahakikishia wananchi hao wa wilaya ya Karatu kwamba vijiji vyote 10 vya wilaya hiyo ambavyo bado havijafikiwa na nishati ya umeme vitafikiwa. Wilaya ya Kataru ina vijiji 57 kati yake vijiji 47 tayari vimeshaunganishiwa umeme.
Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Karatu. Gharama za kuunganishiwa umeme huo amezipunguza kutoka sh. 177,000 hadi sh. 27,000 tu.
Pia Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala hawatalipia fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.
Pia alimuombea kura mgombea ubunge kupitia CCM, Daniel Awaki na kuwaeleza wananchi kuwa mafiga matatu ndiyo yatawezesha jimbo hilo ambalo lilikuwa chini ya wapinzani kwa miaka 25 kusonga mbele.
Amesema, kura ya Rais wampe Dkt.John Magufuli, ubunge kwa Daniel Awaki na madiwani wote wa CCM ili wakaunganishe nguvu kuwaletea maendeleo jimboni humo.