Wengi wetu tunatamani kuyaishi matokeo ya jambo fulani. Lakini, tumejikuta tukishindwa kuyafikia malengo hayo kutokana na sababu kadha wa kadha, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Matokeo hayo ukiweza kuchukua mizani na kuyapima uzito wake utabaini kuwa uwiano wa kukuwezesha kuyafikia malengo yako ulikuwa una nguvu kubwa kuliko matokeo ya kushindwa kuyaelekea matokeo ya hitaji lako.
Pengine, miongoni mwa sababu zinazochangia wengi wetu kushindwa kuyafikia mahitaji au malengo ya ndoto ni kukosa uvumilivu.
Bila kukaa na kutafakari wengi wetu tumekuwa na tabia ya kuyapa kipaumbele mapokeo ya nje kuliko mapokeo ya fikra zetu na imani yetu ya kuziendea ndoto za maisha yetu. Hatua ya kuyapokea matokeo ya nje ambayo yanakuja kwa njia hasi yanachangia kukuondolea uvumilivu, mwishowe unaishia kukata tamaa.
Rejea kuwa, uvumilivu unalipa sana, usikubali kukata tamaa. Mfano wewe ni mwanafunzi, lengo lako ni kuhakikisha unakuwa wa kwanza katika matokeo ya mitihani yako ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kuziendea ndoto zako siku za usoni, ili kufanikisha hayo ni lazima utumie muda wako vizuri kusoma na kupitia maandiko mbalimbali yanayohusiana na masomo yako.
Hatua ambayo itakuwezesha mwisho wa siku wakati wa mtihani uweze kujibu ipasavyo maswali ili uweze kufaulu kwa alama za juu, lakini kutokana na aidha mazingira yanayokuzunguka, mtu au kikundi cha watu kinasababisha wewe kukata tamaa kwa kuingiza hofu kuwa, pengine somo fulani na fulani walikuwa na akili sana, lakini ilipofika siku ya mtihani waliishia kuambulia matokeo mabaya.
Ukiyapa nafasi mapokeo hayo pasipo kufanya tafakari na kujipa ujasiri na uvumilivu wa hali ya juu huku ukichukua hatua, nawe utajikuta unaishia kama hao kina fulani.
Tambua kuwa, si kila unayemwamini ni rafiki yako anaweza kukushauri yaliyomema kila wakati na si kila unayemwamini ni rafiki yako anaweza kukushauri vibaya, sisi binadamu tumetofautiana katika mitazamo na maono ya mambo mbalimbali, hivyo unaweza kupata ushauri wa mapokeo mazuri yakabadilisha historia ya maisha yako na unaweza kupokea mapokeo hasi yakadidimiza historia ya maisha yako.
Jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa, unajipa nafasi, unakuwa mvumilivu, unamuomba Mungu, unapangilia mambo yako kila wakati na unaweza kuanza kutekeleza moja baada ya jingine hatua kwa hatua.
Vivyo hivyo kwa wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima, wafugaji na wengine wengi tusiwe wa kwanza kukata tamaa kwa kila jambo linapojiri, bali tuwe wavumilivu na kujifunza kulingana na mazingira, tambua changamoto unayoiona katika mazingira yako, kwa uvumilivu na kwa tafakari shirikishi baina ya ufahamu wako na maono ya mambo yanayokuzunguka yanaweza kukupa majibu yenye kushangaza wengi kwa kipindi kifupi.
Jiamini, maana kwa uvumilivu wako unaweza kuvuka madaraja ya aina tofauti, iwe ni daraja la hali ngumu katika maisha, uchumi kudumaa, kukosa furaha katika ndoa kutokana na matatizo ya kiafya, elimu, biashara, migogoro na jambo lolote lile, kanuni yako iwe bidii, maombi, uvumilivu na kutokata tamaa.