Rais wa zamani, Silvestre Ntibantunganya ambaye ndiye Mwenyekiti wa ujumbe wa waangalizi kutoka Afrika Mashariki, amesema kuwa uchaguzi mkuu Tanzania ulifanyika kwa kufuata taratibu.
Ujumbe wa waangalizi wa EAC ulikuwa na wajumbe 89 waliosambazwa maeneo mbalimbali kufuatilia mchakato wa upigaji kura, lakini pia utangazaji wa matokeao ya kura hizo.
Kwa mujibu wa BBC, Bwana Ntabitunganya amesema walikutana na wadau wa uchaguzi ikiwemo tume na vyama vya kisiasa na waangalizi wengine.
Ujumbe huo umesema, umeshuhudia hali ya usalama kaika maeneo mbalimbali, watu wakifanya kampeni kwa uhuru kabla ya kuanza shughuli ya upigaji kura.
Katika siku ya kupiga kura vituo vilifunguliwa kwa muda muafaka, masuala ya ya kiufundi yalifanywa kwa weledi.
Waangalizi walishuhudia wapiga kura wakitekeleza wajibu wao bila kutishwa wala hofu.
''Baadhi ya vyama vya siasa au wagombea wamelalamikia kuhusu namna uchaguzi ulivyoandaliwa na namna matokeo yalivyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.Ujumbe wa waangalizi unatoa wito kwa vyama vya kisiasa, kufuata taratibu za kisheria kuonesha kutoridhishwa kwao na matokeo.
"Tunatoa wito kwa vyama vya siasa kuweka mbele maslahi ya Watanzania, ikiwemo usalama na amani na kuepuka vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani,"amesema.
Ujumbe umewapongeza Watanzania kwa busara walioionesha katika shughuli za wakati wa kampeni na uchaguzi kwa kuzingatia kwanza masuala ya amani na usalama.
''Ujumbe unawasisitiza wagombea, vyama vya siasa na wengine wote kuendelea kuimarisha usalama na amani,"amesema mwenyekiti wa ujumbe huo Bw. Ntibantunganya.