WANANCHI WAMUELEZA PROFESA MUHONGO CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI, AWAAHIDI KUZITATUA

Wananchi wa Kijiji cha Mayani Kata ya Tegeruka Wilaya ya Musoma mkoani Mara wamemuomba Mgombea Ubunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo kusaidia kutatua kero ya maji pamoja na kuimarisha huduma ya afya,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Profesa Muhongo akizungumza na wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kijiji cha Tegeruka Nyaminya katika mkutano wake wa kampeni leo Oktoba 9,2020. (Diramakini).
Ni kwa kuwezesha ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Kataryo ndani ya kata hiyo, watakapomchagua katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu kuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Mbali na hayo, wamemuomba pia kuwezesha ujenzi wa sekondari katika Kijiji cha Kataryo ili kuwaondolea adha wanafunzi ambao hutembea umbali mrefu kwenda kusoma Sekondari ya Tegeruka iliyopo mbali pamoja na kuwezesha ujenzi wa Shule Shikizi ya Nyasaenge.

"Wakazi wa Mayani tuna changamoto ya maji tunaomba ipatiwe ufumbuzi maana tunatumia muda mwingi sana kutafuta maji, jambo jingine wananchi wa Kataryo hawana zahanati kwa hiyo hulazimika kwenda Wanyere kutibiwa wanapougua tunaomba tukikuchagua utusaidie zahanati.

"Na pia uwezeshe ujenzi wa Sekondari ya Pili kwenye kata yetu ili wanafunzi wanaotoka Kataryo wasitembee umbali mrefu kuja kusoma Tegeruka, kwani ni mbali sana muda mwingi wanautumia kutembea kwenda shule badala ya kujisomea,"amesema Rosemary Joseph.

Naye Wambura Marwa mkazi wa Mayani amesema, tatizo jingine linalowakabili wananchi ni miundombinu ya barabara ndani ya kata yao ambayo si ya kuridhisha kutokana na kuathiriwa na mvua, hivyo amemuomba Prof. Mubongo kuwezesha utatuzi wake kwa manufaa yao ya kiuchumi pindi watakapomchagua hapo Oktoba 28, mwaka huu.

Wamemueleza hayo katika mkutano wake wa kampeni alioufanya katika Kijiji cha Mayani Kata ya Tegeruka alipotoa fursa ya kusikikiza changamoto zao kabla ya kuomba kura na kunadi sera za chama hicho, ambapo pia amefanya mkutano mwingine katika Kijiji cha Tegeruka Nyaminya, huku changamoto za kijiji hicho zikifanana na za Kijiji cha Mayani kutokana na wananchi hao kuchagua diwani aliyekuwa ametokana na upinzani hivyo kushindwa kutatua kero zao.

Akielezea ufumbuzi wa kero ya maji, Prof. Muhongo amesema kuwa, tatizo hilo linakwenda kutatuliwa na Serikali ya CCM bila kubahatisha, kwani bomba lililopo kwa sasa limechakaa, amesema ilani ya CCM iliyoandaliwa na chama hicho kwa mwaka 2020-2025 inakwenda kutoa ufumbuzi kwani imeaninisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wake.

"Wananchi wa Mayani na Kata ya Tegeruka kwa ujumla, chagueni CCM ndiyo suluhisho la mambo yote, mradi mpya wa Shilingi Bililioni 70.1 fedha zipo hazina, chanzo cha fedha hizo ni sehemu tatu, Serikali ya Saudi Arabia, zingine zinatoka BADEA huu ni ushirikiano wa nchi za Kiarabu na zingine zimetolewa na Serikali ya Tanzania, Mkandarasi aliyekuwa amewekwa wa Taifa la Misri baada ya kumchunguza akawa na mapungufu, Serikali ikatafuta mwingine na tayari ameshapatikana ikiwezekana mwezi Januari ataanza kujenga mradi huo,"amesema.


Prof. Muhongo amesema kuwa, vijiji vitatu vya Kata ya Tegeruka na vijiji vitatu vya Kata ya Mugango vitapata maji, amesema bomba kubwa litajengwa litakuwa na toleo kubwa kusambaza huduma ya maji, huku akisema kuwa ni heshima kubwa kwa Rais Magufuli kuleta mradi huo wa kihistoria ambao utakuwa mwarobaini wa kutatua tatizo la maji kwa wakazi wa Kata ya Tegeruka na maeneo mengine ya Jimbo la Musoma Vijijini.

Kuhusu suala la zahanati, Prof. Muhongo amesema baada ya Uchaguzi Mkuu watamalizia ujenzi wa zahanati 14 ambapo pia amekubali kuhakikisha anawezesha ujenzi wa Zahanati ya Kataryo pamoja na kupanua zahanati ya Masinono kuwa Kituo cha afya kwani Serikali tayari imekwishatoa fedha shilingi milioni 400 kukipanua pamoja na kujenga Hospitali ya Wilaya inayojengwa eneo la Kwikonelo ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini, hivyo amewahakikishia wananchi uhakika wa huduma bora za matibabu.

"Nimekubaliana na maombi yenu yote, kuhusu shule ya Nyasaenge ambayo ni shikizi inajengwa nimekubaliana nanyi kuchangia, nimesema baada ya Uchaguzi kazi inaanza mara moja, lengo ni kufanya Jimbo la Musoma Vijijini liwe na wasomi wengi watakaoleta mapinduzi chanya ya maendeleo, nawaomba sana wananchi pia mtunze kadi zenu vizuri za kupigia kura ili siku ya Uchaguzi mchague mafiga matatu ikiwemo Diwani, Mbunge, na Rais Magufuli wote wa CCM tuchape kazi kwa pamoja," amesema Prof. Muhongo.

Amesisitiza wananchi wa jimbo hilo kutofanya makosa hata kidogo kuchagua wapinzani, kwani Serikali ya CCM imejipambanua kutatua kero zao, kubadilisha maisha yao na kuleta ustawi wa maisha yao huku akitolea mfano kuwa tayari Rais Magufuli ameahidi kujenga barabara ya lami kutoka Busekera kwenda Musoma Mjini yenye urefu wa kilomita 92 jambo ambalo litachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news