Abiy amfukuza Mkuu wa Jeshi, Mkuu wa Usalama, Waziri wa Mambo ya Nje

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed amewatumbua Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Usalama na Waziri wa Mambo ya Nje huku wanajeshi wengi wakiripotiwa kujeruhiwa katika mzozo wa siku tano katika mkoa wa Kaskazini wa Tigray, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ofisi ya Waziri Mkuu ya Mheshimiwa Abiy haikutoa maelezo ya kina juu ya uamuzi huo badala yake taarifa imebainisha kuwa Naibu Waziri Mkuu Demeke Mekonnen ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje huku Naibu Mkuu wa Majeshi,Birhanu Jula akiteuliwa kuwa mkuu kamili.

Wakati huo huo, Temesgen Tiruneh ambaye alikuwa Rais wa Mkoa wa Amhara ameteuliwa kuwa Mkuu mpa wa Idara ya Usalama.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wamemueleza Mwandishi Diramakini kuwa, mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel huenda amechukua hatua hiyo ili kuitaka jamii ya Kimataifa ielewe operesheni ya kijeshi aliyoanzisha wiki iliyopita dhidi ya chama cha Tigray, ambacho amekituhumu kwa kutaka kuvuruga amani si ubabaishaji.

Abiy amesema chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kilichokuwa kinatawala zamani kilikuwa kimefadhili, kufundisha na kuandaa jeshi lolote ambalo lilikuwa tayari kushiriki katika vitendo vya vurugu na haramu ili kukomesha mpito wa kidemokrasia ambao ameufuata nchini humo.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba watu wapatao milioni tisa wako hatarini kupoteza makazi yao huko mkoani Tigray.

Pia umoja huo umeonya kwamba tangazo la hali ya hatari la serikali linachangia ugumu kufikisha chakula na misaada mingine muhimu katika eneo hilo lililopo Kaskazini mwa taifa hilo.

Ripoti zinaonyesha kuwa, watu wa kabila la Tigray wamekuwa wakidhibiti siasa za Ethiopia kwa muda mrefu. Tangu Abiy kuingia madarakani mwaka 2018, wamekuwa wakipambana na juhudi zake za kutaka kupunguza ushawishi wao wa kisiasa nchini humo ili waendelee kutawala.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news