Shule ya Sekondari ya Natiro iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro inahitaji kiasi cha sh.milioni 100 ili kupunguza changamoto zinazoikabili ikiwemo umaliziaji wa jengo la bweni kwa ajili ya wasichana ,ujenzi wa choo cha wavulana, ujenzi wa bwalo na maktaba.
Mkuu wa shule hiyo, Emanueli Mrema ameyasema hayo wakati wa mahafali ya 34 ya shule yaliyofanyika katika shule hiyo iliyopo kijiji cha Natiro kilomita 14 kutoka Moshi Mjini ikiwa na idadi ya wanafunzi 231 kati yao wavulana wakiwa ni 116 na wasichana wakiwa 157.
“Licha ya mafanikio tuliyonayo bado tunakabiliwa na changamoto ambazo ni pamoja na miundombinu isiyokidhi mahitaji ya shule ikiwemo Bweni la wasichana,Choo cha Wavulana na jengo la maktaba pamoja na maeneo mengine ya shule ambayo ni chakavu.
“Ushiriki wa wadau wa elimu katika mahafali haya ni sehemu ya utatuzi wa changamoto zinazoikabili shule yetu, kwani ili kukabiliana na kupunguza makali ya changamoto hizo tunauhitaji wa kiasi cha shilingi milioni 98.3,” amefafanua mwalimu Mrema.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo ambaye pia ni mwanafunzi aliyesoma shule ya sekondari Natiro miaka 20 iliyopita,Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu Benki ya CRDB, Siaophoro Kishimbo akajibu sehemu ya changamoto hizo katika hotuba yake.
“Najua shule ina changamoto nyingi sana ambazo zote tungependa ziweze kutatuliwa na sisi tunaamini kwamba huu ni mwanzo tu wa mashirikiano mazuri ambayo benki yetu itakuwa nayo na shule hii na kwa kuanzia katika ile gharama ya sh. milioni 98 sisi kama benki tutatoa sh.milioni 10,"amesema Kishimbo.




“Tunaamini kwamba hizi fedha hazitoshi, lakini ni kiwango ambacho kinaweza kikasaidia shule kuweza kuimarisha miundombinu yake ili vijana wanaokuja hapa waweze kusoma kwa utulivu na waweze kufaulu kwa viwango vya juu,"ameongeza Kishimbo.
Akitoa nasaha kwa vijana hao Kishimbo amewataka wahitimu hao kutopoteza muda mwingi wawapo katika maeneo ya shule kwani wazazi wamekuwa wakihangaika kutafuta ada ili wao waweze kusoma bila changamoto ya kurejeshwa majumbani kwa ajli ya kukosa ada.
“Kuna msemo unasema jiandae vizuri kabla ya vita ili wakati wa vita ukifika usiwe ni wakati wa wewe kujifunza mbinu mpya bali kuchagua ni silaha gani ya kutumia,usipoteze muda mwingi unapokuwa maeneo haya wazazi wanalipa ada kwa uchungu sana na wengine pengine tunarudishwa ada mara nyingi hatuna,ukipata nafasi itumie nafasi ipasavyo,"amesema.









Kwa upande wake Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini, Chiku Issa amewashauri wahitimu hao kuanza kutengeneza na kushikilia ndoto zao ili kufikia malengo ya nani wanataka kuwa ikiwa ni pamoja na kuondoa matamanio ya ujana ambayo yanaweza kufifisha ndoto zao.
Mgeni rasmi amekabidhi vyeti kwa wahitimu huku Benki ya CRDB ikitoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ikiwa ni pamoja na kufunguliwa akaunti.