Jamii imetakiwa kutambua kuwa zawadi kubwa wanayotakiwa kutoa kwa watoto wao ni kuwapa elimu kwani itawanufaisha kwenye maisha yao ya baadaye, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zuwena Omary ameyasema hayo kwenye mahafali ya tisa ya shule ya awali na msingi New Light iliyopo Mji mdogo wa Mirerani.
Amewataka wazazi na walezi wasiwape watoto wao zawadi ambayo kesho yake hawataifurahia na kuijutia hivyo urithi mzuri ni kuwapatia elimu.
Katibu Tawala Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zuwena Omary akimkabidhi cheti cha kuhitimu darasa la saba kilichotolewa na shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani mhitimu, Gift Lyimo kwenye mahafali ya tisa ya shule hiyo.
Amesema unaweza kumpa mtoto wako zawadi kubwa na ya thamani, lakini baadaye akaipoteza ila akiwa na elimu ni urithi wa maisha yake yote.
Mkurugenzi wa shule ya awali na msingi New Light, Askofu Sommy Severua amesema kupitia elimu mtoto wa kibarua anaweza kupata madaraka makubwa.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Katibu Tawala Wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary akikagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake katika mahafali hayo.
Askofu Sommy amesema, mtoto wa mchimbaji mdogo wa madini miaka ijayo ataweza kuwa Rais wa nchi miaka ijayo endapo atapata elimu.
Amewataka wahitimu wa darasa la saba wa shule hilo kutumia elimu waliyoipata kwa mustakabali wa maisha yao ya baadaye.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema hayo ni mahafali ya sita katika shule hiyo.
Mhitimu wa darasa la saba wa shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Gift Lyimo akikabidhiwa na mama yake Happy Kayumbo zawadi ya keki baada ya mahafali ya tisa ya shule hiyo.
Kobelo amesema, wanafunzi wengi waliohitimu shule hiyo wamepata mafanikio kitaaluma kutokana na msingi mzuri walioupata hapo.
Mmoja kati ya wahitimu wa mahafali hayo Gift Lyimo amesema, ana furaha kubwa kumaliza elimu ya msingi na sasa anasubiria matokeo ya darasa la saba baada ya kufanya mtihani.
Wanafunzi wa shule ya awali na darasa la kwanza wa New Light ya Mji mdogo wa Mirerani wakiwa kwenye mahafali hayo.
Lyimo amesema, ana matumaini makubwa ya kufaulu kwani alipata msingi mzuri kwenye shule hiyo tangu elimu ya awali hadi darasa la saba.
Tags
Habari