DCP Katungu atoa rai kwa wanafunzi Bwawani Sekondari

Wanafunzi na wahitimu wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Bwawani wameaswa kutumia vyema mitandao ya kijamii, kutunza afya zao kwa kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuwapelekea kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na mimba za utotoni,anaripoti Victoria Kazinga (Diramakini) Morogoro.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Kamishina wa Jeshi la Magereza, DCP Jeremiah Katungu, kwenye mahafali ya kumi na saba ya kidato cha nne shule ya sekondari Bwawani iliyoko mkoa wa Pwani, ambapo aliwatahadharisha wanafunzi hao juu ya athari za ugonjwa wa UKIMWI, pamoja na kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya utandawazi.

DCP Katungu amewaasa wanafunzi hao kujiepusha na madawa ya kulevya, na mimba za utotoni kwani athari zake zinaweza kuwasababishia kukatisha ndoto zao za kupata mafanikio katika maisha yao na hivyo kukosa uelekeo na kuwa tegemezi na mzigo kwa jamii.

Naibu Kamishina wa Jeshi la Magereza nchini (DCP) Jeremiah Katungu akikagua gwaride la kikundi cha SKAUTI ambao ni wanafunzi wa shule ya sekondari Bwawani inayosimamiwa na jeshi la Magereza, kwenye mahafali ya kumi na saba yaliyofanyika shuleni hapo. (DIRAMAKINI).

Aidha, amewataka kuepuka matumizi mabaya ya utandawazi yanayoweza kuwapelekea kufanya mambo yasiyofaa na kujiingiza katika uhalifu wa kimtandao, na kuwasisitizia kuhakikisha wakati wote wanafuata maadili mema waliyofundishwa shuleni hapo kwa mustakabali wa maisha yao.

“Nirudie tena kuwaasa wahitimu na wanafunzi wote kwamba mafanikio katika kitu chochote yanategemea kuwa na afya bora, hivyo niwatahadharishe sana juu ya athari za ugonjwa wa UKIMWI, na kuwasihi kuchukua kila aina ya tahadhari kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kupelekea kupata maambukizi,”amesema Katungu.

Nae Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwawani, ACP Anthon Sogoseye amesema, mbali na kupitia kipindi kigumu cha janga la ugonjwa wa Corona (Covid 19) na kusababisha shule zote nchini kufungwa kwa takribani miezi mitatu na nusu, lakini wanatoa shukrani zao kwa Rais Magufuli kuliongoza taifa kwa uthabiti na kumtegemea Mungu.

Wanafunzi kidato cha nne shule ya sekondari Bwawani wakiimba wimbo wa kuwaaga walimu na wanafunzi wenzao katika mahafali yaliyofanyika shuleni hapo. (DIRAMAKINI).

Amesema, mbali na wanafunzi shuleni hapo kufanya vizuri kitaaluma lakini pia wanalelewa kwa nidhamu ya hali ya juu, pamoja na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kutunza mazingira kwa kupanda miti ya matunda na kivuli kupitia vikundi vyao vya SKAUTI na MALI HAI.

Akizungumzia, changamoto mbalimbali zinazo ikabili shule hiyo, Sogoseye amesema ni pamoja na baadhi ya wazazi kutolipa ada kikamilifu na kwa wakati muafaka, hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo yao na kurudi nyumbani kufuata ada, na hivyo kuwaathiri kitaaluma na wakati mwingine kisaikolojia.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwawani, ACP Anthon Sogoseye (aliyesimama) akizungumza katika mahafali ya kuwaaga kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo.(DIRAMAKINI).

Kwa upande wa wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo akiwemo Isack Magelanga wamewaasa vijana wenzao kutumia mitandao ya kijamii kwa kujifunza mambo mazuri na yenye faida kama kilimo na ufugaji na kuacha kujikita kwenye mambo yasiyokuwa na manufaa kwenye maisha yao.

Wanafuzi 146 kati yao wavulana ni 90 na wasichana 56 wa kidato cha nne shuleni hapo ambao wanatarajiwa kuanza mitihani Novemba 23, 2020, huku mahafali hayo yakiwa ni ya kumi na saba toka mfumo wa shule hiyo ulipobadilishwa mwaka 2003 kutoka kudahili wanafunzi watumishi wa Jeshi la Magereza na kuwa sekondari ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news