Zoezi hili litafanyika chini ya Idara ya Afya Kiteto ambapo imeelezwa kuwa wengi wa wananchi wamekaidi kuchimba vyoo na kuvitumia jambo ambalo ni hatari kiafya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto,Tamimu Kambona akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Njoro amesema, magonjwa ya milipuko yanaweza kujitokeza mvua za masika zitakapoanza kutokana na wengi wao kutokuwa na vyoo.
"Serikali tumetoa elimu ya kutosha kwa wananchi wote, tumejenga vyoo vya mfano na namna ya kuvitumia, inaonekana wengi wao wamekaidi, sasa tumeamua sheria itafuata mkondo wake muzuia maafa,"amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto,Tamim Kambona akizindua Kampeni ya Usafi wa Mazingira Kata ya Njoro. |
"Tutatumia Jeshi la Polisi, tutawakamata wale wote ambao hawana vyoo na tutaanza na Kata ya Njoro tutazunguka wilaya nzima ya Kiteto, kwani tusipofanya hivyo madhara makubwa yanaweza kujitokeza,"amesema.
Amesema, zipo mila potofu kwa baadhi ya makabila kama Wamasai wao hawana utamaduni kabisa wa kuwa na vyoo kwenye makazi yao, "naagiza kupitia mkutano huu wachimbe vyoo na ole wao watakaokutwa hawana vyoo,"alisema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Njoro, Saidi Sasu akizungumza katika mkutano huo amesema, atahakikisha anatoa ushirikiano ili sheria ifuate mkondo wake kwa wananchi watakaokaidi.
Amesema, suala la vyoo sio jambo geni kila mara madhara yamekuwa yakijitokeza kwa wananchi huku wakiendelea kuilaumu Serikali.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto, Pascal Mbota amesema, madhara makubwa yamekuwa yakijitokeza kama vile maafa kutokana na magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu na kuwataka wananchi kubadilika.
"Mwaka juzi tulipoteza watu wengi kwa kipindupindu kule Njaniodo Kata ya Partimbo, hii ilitokana na wengi kunywa maji machafu yaliyotuama huku wakiwa hawana vyoo,"amesema Mbota.