Mchezaji nyota wa zamani wa kandanda Diego Maradona amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 60.
Kiungo huyo mshambuliaji wa Argentina awali mwezi huu alifanyiwa upasuaji wa ubongo ambao madaktari walimwambia ulifaulu.Baada ya upasuaji huo, ilitangazwa kuwa Maradona angeanza matibabu ya uraibu wa pombe.
Maradona ni moja ya wachezaji bora zaidi wa kandanda kuwahi kutokea. Mwaka 1986 akiwa nahodha wa Argentina, aliliongoza Taifa lake kushinda Kombe la Dunia nchini Mexico huku akionesha uwezo binafsi mkubwa katika ushindi huo.
Alizichezea klabu za Barcelona ya Uhispania na Napoli ya Italia. Akiwa na Napoli alinyakua ubingwa wa ligi ya Serie A kwa misimu miwili.
Maradona aliifungia Argentina magoli 34 katika michezo 91, akishiriki michuano minne ya Kombe la Dunia.