Dkt.Abbasi akagua uwanja, Polisi waonya mashabiki wang'oa viti

Leo Novemba 6, 2020 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi ametembelea na kukagua maandalizi ya Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya watani wa jadi Simba SC na Yanga SC inayotarajiwa kuchezwa kesho Novemba 7, 2020, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt. Abbasi amewahakikishia mashabiki kesho itakuwa zaidi ya burudani kwani usalama umeimarishwa na pia amewahimiza mashabiki na wapenzi wa soka kukata tiketi mapema na kufika uwanjani mapema.

Pia Dkt. Abbasi amewahakikishia uwanja huo kesho unakwenda kuwa sehemu ya sherehe kubwa na mashabiki watapata chakula ndani ya uwanja kwa bei ya kawaida na kutakuwa na burudani ya kiwango cha juu kutoka kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao watausindikiza mchezo huo.
 
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa ametoa onyo kali kwa wale watakaothubutu kung’oa viti na kufanya vurugu kwenye mchezo huo.

Msimu wa 2016/17, timu hizo zilicheza ambapo zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Yanga lilifungwa na Amisi Tambwe ambapo mashabiki wa Simba SC walifanya vurugu na kung’oa viti.

Kamanda Mambosasa amesema kuwa, kwenye mpira wa miguu kuna matokeo matatu hivyo mashabiki wakubaliane na lolote litakalotokea katika mchuano huo wa kesho baina ya wekundu wa Msimbazi Simba SC na Wana Jangawani Yanga SC.

“Mpira una matokeo matatu kuna ushindi, kushindwa na kutoa sare na wajiepushe na mihemko ya kishabiki, mara nyingi baada ya kushindwa watu wanahangaika kung’oa viti kwani viti vinakosa gani, leo umeshindwa na kesho utashinda, suala la kuharibu mali na kufanya vurugu ni uchwara kwenye ushabiki, niwaombe wawe watulivu, wanadi timu zao na wajiandae kwa matokeo,”amesema.
 
Aidha, Yanga SC inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Simba SC katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news