Leo Novemba 24, 2020 wabunge 19 wa Viti Maalum wakiongozwa na Halima Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameapishwa nje ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Wengine ni Asia Mohamed, Felista Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Simon, Anatropia Theonest,Salome Makamba, Conchester Lwamraza, Grace Tendega, Ester Matiko,Secilia Pareso,Ester Bulaya,Agnes Kaiza,Nusrat Hanje,Jesca Kishoa,Hawa Mwaifunga na Tunza Malapo.Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai amesema, zoezi hilo amelifanya kwa mujibu wa Ibara ya 78 (i) ikisomwa na ibara ya 69(i)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Amesema, vyama vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kupata angalau asilimia tano ya kura zote halali za wabunge, inaelekeza vitapendekeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) majina ya wanawake kwa kuzingatia uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi wa wabunge waliopendekezwa wawe wa wabunge wa viti maalum kupitia vyama hivyo nchini.
"Novemba 20, mwaka huu nimepokea barua kutoka NEC yenye maelezo kuwa imefanya uteuzi wa wabunge wa viti maalum vya wanawake 19 kwa mwaka 2020, hivyo ibara ya 68 ya Katiba imeweka masharti kwamba kila mbunge atatakiwa kuapishwa na Spika kiapo cha uaminifu kabla hajaanza kushiriki shughuli za Bunge
Aidha kanuni ya 30 (2)(b) ya kanuni za Bunge inatoa ufafanuzi zaidi kuhusu kiapo cha wabunge kwa kipindi ambacho kunakuwa hakuna mkutano wa bunge unaoendelea. Kama hakuna mkutano wa Bunge unaoendelea kanuni inaeleza bila kujali masharti ya fasili ya kwanza endapo mbunge atachaguliwa,baada ya uchaguzi Spika atamwapisha katika eneo litakalopangwa na Spika iwapo hakuna mkutano wa Bunge unaondelea na baadaye Spika atatoa taarifa bungeni kwenye kikao cha kwanza cha mkutano wa Bunge uaofuata
"Kwa hiyo tunaochanganya kwamba kila mbunge ni lazima aapishwe mbele ya Bunge, kanuni inasema ataapisha mbele ya Spika na kama hakuna mkutano unaoendelea kama ilivyo hivi sasa Spika atachagua eneo litakalotosha na linafaa kwa kazi hiyo na kwa hiyo nimechagua eneo hili na ndio maana tumeifanya hii kazi hapa tulipo.Kwa masharti hayo wabunge wanaweza kuapishwa muda wowote na mahali popote kwa kadri itkavyopangwa na Spika.
"Utaratibu huu mpya unatokana na Bunge la 11 kuona ipo haja ya kutatua changamoto ya wabunge wanaochaguliwa au kuteuliwa kuchelewa kuanza kutekeleza majukumu yao kwa ajili ya kusuburi kuapishwa wakati kiu ya wananchi ni kuona kwamba mara mbunge anapopatikana anaanza kutekeleza majukumu yake bila kuchelewa.
"Jambo hili hapo awali lilikuwa gumu kwa kuwa ilikuwa lazima mbunge asubiri kwanza aapishwe kwenye mkutano wa Bunge unaofuata na utaratibu huu wa kuapishwa wabunge wakati hakuna Bunge linaloendelea unatumika mahali pengi katika mabunge yenye utamaduni kama wa kwetu lengo ni kuwaapisha wabunge pasipo kuchelewa na kuwawezesha kuanza kutekeleza maujukumu ya kibunge kwa kuchukua shida za wananchi na kuzifanyia kazi kwa haraka,"amefafanua kwa kina Spika Ndugai.