HGWT lawapa elimu wasichana waliokimbilia Nyumba Salama

NA FRESHA KINASA

Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalotoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni kupitia Kituo cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama na Nyumba ya Matumaini Mugumu Wilaya ya Serengeti, limewapa elimu wasichana 43 waliokimbilia katika vituo hivyo kwa ajili ya kuhifadhiwa kufuatia wazazi wao kutaka kuwakeketa.

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly akiwa na baadhi ya wasichana wanaohifadhiwa Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu Serengeti kufuatia kukimbia kukeketwa katika familia zao. (Picha na HGWT,Diramakini).

Wasichana hao walipokelewa katika vituo hivyo hivi karibuni ambapo miongoni mwao ni wahitimu wa darasa la saba na wengine ni wanafunzi na 41 ni kutoka Wilaya ya Tarime ambao wamehifadhiwa Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama na wawili kutoka Wilaya ya Serengeti wamehifadhiwa Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu Serengeti.

Elimu waliyopewa ni ya ukatili wa kijinsia, elimu juu ya haki zao, kuwaondolea woga na kuwajenga kisaikolojia, ikizingatiwa kuwa mwezi Desemba baadhi ya koo za Kikurya ukeketa wakiwa likizo, hivyo kwa muda wote watapata hifadhi na huduma zingine za kibinadamu hadi pale msimu wa ukeketaji utakapomalizika na majadiliano ya pamoja baina ya wazazi, Serikali na shirika hilo kufanyika ili wawapokee kwa masharti ya kutowafanyia ukeketaji.

Ameyasema hayo Mkuu wa Kituo Cha Nyumba ya Matumaini kinachomilikiwa na shirika hilo kilichopo Mugumu Wilaya ya Serengeti, Daniel Misoji wakati akizungumza na DIRAMAKINI na kusisitiza kuwa, wanaendelea na uelimishaji kwa jamii ili watambue madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike na kufanya uamzi thabiti wa kuachana na mila hiyo.

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT), Rhobi Samwelly amesema kuwa, kila mmoja anawajibu wa kuunga mkono juhudi za kupambana na ukeketaji kwa kuwafichua wahusika bila kuwaonea aibu ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kuwajibishwa kwani ukeketaji ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Rhobi ameongeza kuwa, ukeketaji una madhara kwa watoto wa kike ikiwemo kukatisha masomo yao, matatizo ya kisaikolojia kama vile msongo wa mawazo, maumivu makali wakati wa kukeketwa, kutokwa damu nyingi hali ambayo inaweza kupelekea kifo akaomba jukumu la kuwalinda lifanywe na kila mmoja na si kuiachia jukumu hilo Serikali ama mashirika kutekeleza wajibu huo.

"Tuwalinde watoto wa kike kama mboni ya jicho, tunao mfano mzuri wa viongozi wa kike wakiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, hawa wametokana na matunda ya elimu ndio maana leo ni viongozi wetu tena wanafanya kazi vizuri sana. Niombe jamii inayokeketa iache, maana mtoto akikeketwa ni maandalizi ya kumuozesha na kama ni mwanafunzi lazima atakatisha masomo yake hii ni hasara katika kujenga kizazi kijacho,"amesema Rhobi.

Shaban Julius na Editha Marco wakazi Mugumu Wilaya Serengeti wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamesema wanapongeza kazi kubwa inayofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwani imechangia kwa kiwango kikubwa kuwaokoa wasichana wengi dhidi ya ukeketaji pamoja na kuongeza uelewa kwa wananchi kutokana na elimu ambayo wamekuwa wakiitoa kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana,wazee, shuleni na katika mikutano ya hadhara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news