NA FRESHA KINASA
Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojihusisha na kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni katika Wilaya ya Butiama na Serengeti kwa kushirikiana na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii wilayani Serengeti Mkoa wa Mara Novemba 26, 2020 wamezindua maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika Kijiji cha Bunchugu Kata ya Sedeko Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kwa kuwaelimisha Vijana na Wazee wa kimila.
Hidaya Mkaruka kutoka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Serengeti akitoa elimu ya madhara ya ukatili kwa Wazee wa kimila kijiji cha Bunchugu Kata ya Sedeko Wilaya ya Serengeti.(Diramakini).
Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka ambapo baada ya kukutana na wazee na vijana hao wametoa elimu ya ukatili wa kijinsia hususan madhara ya ukeketaji,huku wakiitaka Jamii kuwalinda Watoto wa kike, kuwathamini kwa kuwapa fursa ya elimu katika kuwaandaa waje watoe mchango wa maendeleo katika jamii yao sambamba na kuchangia kwa dhati ukuaji wa uchumi wa nchi kwa siku za usoni.
Shirika hilo chini ya Mkurugenzi wake Rhobi Samwelly ambalo lina vituo viwili vya kutoa hifadhi kikiwemo cha Nyumba ya Matumaini cha Mugumu Wilaya ya Serengeti na Nyumba Salama kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama, linalenga kuwafikia wananchi wengi kipindi hiki katika maeneo yao, ili kuwafikishia elimu hiyo na kuweka mikakati ya pamoja ya kutokomeza vitendo hivyo ambavyo vinatajwa kufanyika hususan mwezi Desemba ambapo wanafunzi huwa likizo na wazazi hutumia mwanya huo kuwakeketa, huku koo za Kikurya ikiwemo Wailegi, Wanyabasi, Wakenye Walinchoka wakitajwa kufanya vitendo hivyo.
Emmanuely Good luck ni Afisa Uelimishaji Jamii wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania amesema kuwa Katika maadhimisho ya siku 16 mwaka huu, Shirika hilo litatoa elimu Katika vijiji vya Wilaya ya Serengeti na Butiama kufikisha elimu hiyo, na kwamba lengo ni kuona jamii ikishiriki kikamilifu kutokomeza ukatili kwa watoto wa kike ikiwemo ndoa za utotoni na ukeketaji ambao umekuwa ukirudisha nyuma maendeleo ya watoto wa kike kufikia malengo yao kwa kukeketwa ili kuozeshwa katika umri mdogo.
"Shirika tunatambua kwamba, mtoto wa kike akipewa fursa ya elimu ana nafasi kubwa ya kubadilisha jamii yake, kumkeketa ni kumwandaa kumuozesha na Serikali haitaki akatishwe ndoto zake, maadhimisho ya mwaka huu tumekusudia kuyafikia makundi yote kuyapa elimu na kujua sababu ambazo bado zinawafanya waendelee kuwakeketa mabinti licha ya Serikali na wadau kupambana na mila hii iliyopitwa na wakati, lakini pia ina madhara makubwa kwao, tuweke mikakati ya pamoja namna ya kudhibiti vitendo hivi ambavyo mwezi Desemba hufanywa,"amesema Good Luck.
Naye Hidaya Mkaruka kutoka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Serengeti akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, amewaomba wazee wa kimila na vijana wote kuhakikisha kwamba wanakuwa sehemu muhimu ya kushiriki katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo kuwafichua wanaojihusisha na ukeketaji kabla hawajatekeleza azma yao ili kulinda haki, heshima, utu na thamani ya mtoto wa kike kama ambavyo katiba ya nchi na haki za binadamu zinaelekeza.
Marwa Nturu ni miongoni mwa wazee wa kimila na mkazi wa Kijiji cha Bunchugu amesema ukeketaji una madhara kwa watoto wa kike na hauna faida yoyote na kwamba, umekuwa ukifanywa kwa madai ya kuleta heshima kwenye familia husika, kudumisha mila na sehemu ya kujipatia kipato pindi binti anapokeketwa ngariba hupewa fadha, akashauri ukeketaji upingwe kutokana na madhara ya kutokwa damu nyingi wakati binti akikeketwa na hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza maisha.
Chacha Willison na Fabian Faustine wakazi wa Serengeti wakizungumza kwa nyakati tofauti wamelishukuru Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwa jinsi ambavyo limekuwa mstari wa mbele kutetea watoto wa kike dhidi ya ukatili hususan kuwapa hifadhi wanapokimbilia katika vituo vya shirika hilo kutafuta hifadhi wakati ambao wazazi na walezi wao wanapokuwa wakitaka kuwakeketa.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly akizungumza hivi karibuni amesema shirika limepokea watoto 43 waliokimbia ukeketaji kutoka kwenye familia zao ambapo 41 ni kutoka Tarime na wamehifadhiwa kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama na Wawili kutoka Serengeti ambao wamehifadhiwa kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu Serengeti.