Serikali ya Israel imeanza jaribio la chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ambapo kama itafanikiwa itaanza kutumiwa na umma mwishoni mwa msimu ujao wa kiangazi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, watu wanane waliojitolea watashiriki awamu ya mwanzo ya jaribio hilo, ambapo wanaweza kuongezwa hadi watu 960 ifikapo Desemba,mwaka huu.
Endapo majaribio hayo ya mwanzo yatakuwa yamefanikiwa, hatua ya tatu itahusisha watu 30,000 ambayo imepangwa kufanyika kati ya Aprili na Mei,2021.
Aidha,Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kibaolojia ya Israel, Shmuel Shapira amesema wapo katika hatua ya mwisho.
Hata hivyo, Israel imeripoti visa vipya 674, kutoka katika kilele cha zaidi ya watu 9,000 katika wiki kadhaa zilizopita na imeripoti vifo 2,541 vilivyotokana na Covid-19.