Jafo aagiza barabara mji wa Serikali zikamilike kwa wakati

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewataka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wanaosimamia ujenzi barabara ya mzunguko katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliowekwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Jafo ametoa agizo hilo wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa barabara hizo zinazoendelea kujengwa kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma na kubaini ujenzi kuwa nyuma ya muda uliowekwa kwa asilimia mbili.

“Mmeniambia changamoto ni mvua na ugonjwa wa Corona, kwangu mimi sioni sababu ya msingi kati ya hizo mlizotaja sababu mpaka sasa hivi msimu wa mvua bado haujaanza na hakuna mvua kubwa iliyonyesha ya kusababisha ucheleweshaji wa ujenzi huu kwa namna yeyote.

"Ugonjwa wa Corona pia sioni ni kwa namna gani ulivyoathiri ujenzi huu, ninachotaka ni barabara hii kukamilika kwa wakati uliopangwa,”amesema Jafo.

"Ninachokiona hapa ni kuwa huyu Mkandarasi ana kazi nyingi kitu kinachompelekea kugawanya vifaa na mitambo yake kwenye site zingine na kusababisha baadhi ya maeneo kazi kudorora kutokana na uchache wa vifaa,"ameongeza Jafo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 51.2 Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seif amesema ujenzi umefikia asilimia 48 ambapo kwa mujibu wa ratiba ilitakiwa kufikia asilimia 50.

Mhandishi Seif ameongeza kuwa, ujenzi wa barabara hizo unahusisha ujenzi wa barabara za njia nne zenye urefu wa kilomita 11.2, ujenzi wa njia mbili zenye urefu wa kilomita 28.8, ujenzi wa kalavati, mifereji ya maji ya mvua, barabara za waenda kwa miguu pamoja na taa za barabarani.

Mradi wa ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba unatekelezwa na Mkandarasi China Hainan International Cooperation Co. Ltd (CHICO) kwa gharama ya sh.Bilioni 88.1 na muda wa ujenzi ni miezi 18 ambapo utakamilika Julai 31,2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news