Kikosi Maalum chenye dhamana ya kusimamia ulinzi wa Rais na majukumu mengine nchini Marekani kimetajwa kumuongezea ulinzi mkubwa wa siri mgombea Urais wa Chama cha Democratic, Joe Biden, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kwa sharti la kutoandikwa jina lake mmoja wa maafisa kutoka Wilmington ameudokeza mtandao huu kuwa, ulinzi wa mgombea huyo umeimarishwa zaidi baada ya kuonekana kuwa, lolote linaweza kutokea.
"Hii ni ishara kwamba kuna lolote linaweza kutokea kuanzia sasa, kuna viashiria vya wazi kabisa kuwa, ushindi hadi sasa upo mikononi mwa Joe, hivyo Joe kuimarishiwa ulinzi inaashiria kuna jambo. Pengine ni jambo la subira, tutazidi kujuzana zaidi," amefafanua Afisa huyo katika mahojiano na Mwandishi Diramakini kutoka mjini humo.
Licha ya ishara hiyo, Msemaji wa Kikosi hicho, Catherine Milhoan amebatilisha madai hayo na kusema kwa kifupi kuwa, idara hiyo haitajadili juu ya mipango ya ulinzi kwa Rais au mgombea yoyote katika nafasi hiyo.
Hata hivyo, matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu nchini Marekani yanaonyesha kuwa, Joe Biden amemuacha nyuma mgombea urais kupitia Chama cha Republican ambaye pia ni Rais wa Marekani, Donald Trump.