Prof.Msanjila afungua fursa kwa AGA Bullion kuwekeza kwenye Sekta ya Madini nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila leo Novemba 12, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na kampuni ya AGA Bullion kutoka nchini Uturuki ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma ambayo imeonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini nchini, anaripoti Steven Nyamiti (WM) Dodoma.
Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila akizungumza na watendaji wa kampuni hiyo walipokutana Novemba 12, 2020 jijini Dodoma. [WIZARA YA MADINI].
 
Katika kikao hicho kilichofanyika ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, Katibu Mkuu Msanjila ameileza kampuni hiyo uwepo wa masoko ya madini yaliyoanzishwa kila mkoa nchini hususani ile yenye uzalishaji mkubwa wa madini ikiwa ni pamoja na Mkoa wa  Geita, Mwanza, Kahama na Chunya, Arusha na kwingineko ambako AGA Bullion wataweza kuwekeza, kununua na kuuza dhahabu kwenye masoko ya nje.  

Prof. Msanjila ameitaka Kampuni ya AGA Bullion kuwafikia wachimbaji wadogo na wa kati kwa kuwapa uzoefu wa uwekezaji katika sekta ya madini na kupendekeza kutembelea mgodi wa dhahabu wa Geita na Busolwa, mgodi wa kati unaofanya uwekezaji katika uchimbaji wa madini ya dhahabu vizuri nchini.

Mkurugenzi mwanzilishi wa Kampuni ya AGA Bullion akizungumza jambo mbele ya Katibu Mkuu na wadau wengine wa Sekta ya Madini leo Novemba 12, 2020 jijini Dodoma. [WIZARA YA MADINI].
 
Amesisitiza, uwekezaji unaopangwa kufanywa na Kampuni ya AGA Bullion usilenge kwenye biashara ya madini ya dhahabu pekee bali kwenye madini mengine yanayopatikana nchini yakiwemo madini ya Tanzanite yanayopatikana mkoani Manyara, pia  kuomba  leseni ya uchimbaji  ili waweze kuchimba  madini  nchini.

Prof. Msanjila ameitaka Kampuni ya Aga Bullion kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya Madini  wakiwemo  Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambao hutoa huduma na ushauri wa kitaalam kwa wachimbaji wadogo, uchenjua dhahabu, kununua na kuuza kutokana na uwepo wa Refinery mkoani Mwanza itakayoanza shughuli mwezi Disemba, 2020.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini akizungumza jambo wakati alipokutana na watendaji wa kampuni ya AGA Bullion Novemba 12, 2020 Jijini Dodoma. [WIZARA YA MADINI]. 
 
Pia amewataka kwenda Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kupata taarifa za kitafiti ndani ya nchi, ramani za kijiolojia zinazoonyesha sehemu zenye madini na Tume ya Madini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwanzilishi wa AGA Bullion, Sarp Tarhanaci amemweleza  Prof. Msanjila kuwa Kampuni ya Aga Billion inamiliki viwanda viwili vya usafirishaji wa dhahabu (Refineries) katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (Dubai) na Uturuki.

Pia, ameelezea uzoefu wao katika ununuzi wa dhahabu kutoka katika mataifa mbalimbali kama vile Ghana, Burkina Faso, Peru, Malaysia na Uturuki.

Akizungumzia juu ya maelekezo ya kukutana na wadau wengine wa Sekta ya Madini, Tarhanaci amesema tayari kampuni hiyo Novemba 10, 2020 ilikutana na kufanya mazungumzo na Chama cha Wachimbaji Wakubwa wa Madini (Tanzania Chambers of Mines (TCME),  ambapo imepokea taarifa za uzalishaji na mauzo ya dhahabu.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (wa nne toka kulia),watumishi toka Wizara ya Madini pamoja na watendaji toka Kampuni ya Aga Bullion walipokutana jijini Dodoma leo Novemba 12, 2020. Kulia toka kwa Katibu Mkuu ni Mkurugenzi Mwanzilishi wa Kampuni ya AGA Bullion, Sarp Tarhanaci. [WIZARA YA MADINI].

Pia Novemba 11, 2020  ilikutana na Mkurugenzi wa Masoko ya Kifedha wa Benki Kuu ya Tanzania ili kueleza nia yake ya kutaka kutoa huduma ya usafirishaji wa dhahabu, bima na kutafuta masoko ya kimataifa ya dhahabu iliyosafirishwa kwa gharama ya asilimia 0.5 hadi asilimia 0.8 ya thamani ya madini hayo.

Aidha, amesema, kampuni ya AGA Bullion kwa kiasi inayo dhamira ya kufanya biashara ya madini ya dhahabu kutoka wa wachimbaji wadogo, wachimbaji wa kati ikiwemo kuwawezesha kwa kuwapa mitaji ya fedha ili waweze kuzalisha zaidi na kutoa mafunzo kwa wachimbaji na kukutana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA) ili waweze kujadili mambo mbalimbali kwa pamoja.

Aidha, amezungumzia nia ya kampuni hiyo kusaidia viwanda vya uongezaji thamani madini ya dhahabu (jewellery industry) kwa kutengeneza bidhaa zake kama vile pete, hereni na mikufu.

Viongozi wengine waandamizi wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Kamishina wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Issa Nchasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news