Uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mdandu wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe umeiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka miundombinu ya kitalii katika eneo la kihistoria lenye andaki,kituo cha mawasiliano ya simu,Mahakama ya mkoloni pamoja na mti uliotumika kunyongea watumwa kipindi cha utawala wa kikoloni.
Mti huo uliopewa jina la Mnzombe ambao ndiyo asili ya jina la mkoa wa Njombe umesalia kuwa na historia kubwa kwa wakazi wa mkoa huo na kuitaka serikali kuona namna ya kuweka miundombinu itakayowavutia watalii kutembelea eneo hilo.
Frank Yohanes Munuo ni mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mdandu chenye mikasa isiyosahaulika karne na karne anatoa historia fupi juu ya namna eneo hili lilivyokuwa likitumika na mkoloni kipindi cha utawala wa Mjerumani na Muingereza.
Anasema, kumbukumbu za kihistoria ukiwemo mti wa Nzombe,Mahakama na Kituo cha mawasiliano kilichotumika na watawala wa kikoloni kwa sasa zipo hatarini kupotea jambo ambalo linawasukuma wakazi wa kijiji hicho kuona ulazima wa kuboresha na kulitangaza eneo hilo ili litambuliwe kama kivutio cha kitalii.
Samweli Kajiba mtalii aliyetoka mkoani Mbeya kwa lengo la kujionea maajabu ya kihistoria katika eneo hilo nae anaonyesha kutoridhishwa na mazingira yaliopo katika eneo hilo lenye kumbukumbu nyingi ,anasema eneo hilo ni ,muhimu kutunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Tags
Habari