Leo Novemba 5,2020 ndiyo ukomo wa Baraza la Mawaziri katika kutekeleza majukumu yao nchini Tanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mawaziri na Manaibu Waziri wa wizara mbalimbali wanafikia ukomo baada ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika muhula wake wa kwanza wa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015 hadi 2020 kutekeleza majukumu mbalimbali ambayo yamewezesha Serikali kufikia matokeo chanya katika sekta na idara mbalimbali.
Aidha, ukomo huo ambao ni wa mapema leo, utafikiwa wakati macho na masikio ya Watanzania yakielekezwa makao makuu ya nchi jijini Dodoma kushuhudia tukio la kihistoria la kuapishwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli baada ya ushindi wa kishindo alioupata wa asilimia 84.4 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Awali Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya kuapishwa kwa Rais Mteule, Dkt. Magufuli amesema, ukomo huo wa mawaziri utafikiwa leo.
Msemaji huyo wa Serikali amebainisha kuwa,kisheria Baraza la Mawazili la 2015-2020 mwisho wake ni mara tu Rais Mteule atakapoapishwa kushika kipindi chake cha pili cha miaka mitano.
Amesema, baada ya hapo majukumu yote yatafanywa na makatibu wakuu wa wizara hadi Rais atakapotangaza baraza jipya. Rais Mteule Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anaapishwa leo katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo viongozi mashuhuri, mabalozi, wageni kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo Watanzania watahudhuria sherehe hiyo kubwa.
Tags
Habari