Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli leo Novemba 5, 2020 ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili cha miaka mitano baada ya kipindi cha kwanza cha miaka mitano kumalizika, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Dkt.Magufuli ameapishwa kushika wadhifa huo baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 ambapo alipata jumla ya kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote zilizopigwa kwa wagombea 15 waliokuwa wanawania kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Dkt. Magufuli ameapishwa pamoja na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ameapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia kuna Mawaziri, Mabalozi, Wawakilishi wa
Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya za Kikanda, viongozi wakuu wa vyombo
vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa
kikiwemo chama tawala nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
viongozi wa sekta binafsi.
Viongozi wakuu wa nchi waliohudhuria
sherehe hizo ni Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni,
Rais wa Umoja wa Visiwa vya Komoro, Mheshimiwa Azali Assoumani, Rais wa Jamhuri
ya Zimbabwe, Mheshimiwa Emerson Mnangagwa na pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Botswana, Mheshimiwa Slumber Tsogwane.
Ambaye amemwakilisha Rais wa nchi hiyo
Mheshimiwa Mokgweetsi Masisi, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Mheshimiwa Carlos Agostinho
Rosario ambaye amemwakilisha Rais wa Msumbiji Mheshimiwa Filipe Nyusi na Naibu
Waziri Mkuu wa Qatar Sultan bin Saad Al Muraikhi aliyemwakilisha
Mtawala wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Than.
Akizungumza baada ya kuapishwa kwake, Mheshimiwa Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini na amewahakikishia kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo kati yake na nchi hizo.
Mheshimiwa Rais Magufuli amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wote wa Tanzania kwa kuhakikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unafanyika na kukamilika kwa amani na utulivu, jambo ambalo limeendelea kudhihirisha kuwa Tanzania sio tu kisiwa cha amani bali pia ni kitovu cha demokrasia.
Amekishukuru chama chake cha CCM kwa kufanya kampeni nzuri zilizowezesha kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao sasa wanakwenda kubeba jukumu la kuwahudumia wananchi wa Tanzania kama walivyoahidi.
Katika sherehe hizo Wakuu wa Nchi wamepata nafasi ya kutoa salamu ambapo Mhe. Rais Museveni pamoja na kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuchaguliwa na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka Watanzania hasa vijana kurejea madhumuni ya uhuru uliopiganiwa na waasisi akiwemo Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere huku akiwataka kujiepusha kuwa vibaraka wa mabeberu na kufanya kazi ili kujitegemea na kujenga ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Mnangagwa wa Zimbabwe ameishukuru Tanzania ambayo amesema Zimbabwe inaiona kama Baba na Mama huku akitambua juhudi za kuanzia Hayati Mwl. Nyerere hadi Mhe. Rais Magufuli ambao wamekuwa mstari wa mbele kuipigania Zimbabwe bila kuchoka.