Mabingwa watetezi, Simba SC leo wameishushia kichapo kikali, Coastal Union ya Tanga baada ya kuibamiza mabao 7-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Ushindi huo unawafanya Wekundu hao wa Msimbazi wafikishe alama 23, ingawa wanaendelea kubaki nafasi ya tatu wakizidiwa alama mbili na vinara, Azam FC baada ya wote kucheza mechi 11.
Katika mchezo wa leo, Nahodha John Raphael Bocco alifunga mabao matatu peke yake yote kipindi cha kwanza na mengine yakafungwa na viungo Mzambia Clatous Chama mawili, Mghana Bernard Morrison na mzawa Hassan Dilunga, kila mmoja moja.
Dilunga dakika ya nane ndiye aliyefungua hesabu ya mabao hayo akimalizia pasi ya Bocco aliyefuatia kufunga dakika ya 24, 29 na 38 kabla ya Morrison kufunga dakika ya 45 na Chama dakika ya 62 na Dk 85.
Wakati huo huo, mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Reliant Lusajo dakika ya 57 limeipa ushindi wa 1-0 KMC dhidi ya Azam FC Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Na Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, mabao ya Meshack Abraham dakika ya 72 na Paul Nonga dakika ya 84 yameipa ushindi wa 2-0 Gwambina FC dhidi ya JKT Tanzania, wakati Polisi Tanzania imelazimishwa sare ya 0-0 na Ihefu SC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jiji la Dar es Salaam.
Kikosi cha Coastal Union kilikuwa kimeundwa na Abubakar Abbas, Hassan Kibailo, Hance Msonga, Peter Mwangosi/ Humid Mbuki dk55, Seif Bihaki, Abdul Sultan, Salum Ally, Mtenje Albano, Raizin Hafidh, Issa Abushehe na Hamad Majimengi/Paul David dakika ya 55.
Kwa upande wa kikosi cha Simba SC kiliundwa na Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango/Ibrahim Ame65, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Hassan Dilunga/Francis Kahata dk65, Said Ndemla, John Bocco/Ibrahim Ajibu dk46, Clatous Chama na Bernard Morrison.