Yanga SC yakwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara

Klabu ya Yanga imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Azam FC leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
 Deus Kaseke ndiye aliyeibuka shujaa wa Yanga SC, baada ya kuifungia klabu hiyo bao pekee dakika ya 48 baada ya kazi nzuri kutoka mita 14 ambayo ilimshinda kipa David Mapigano Kissu kufuatia pasi nzuri ya Yacpouba Sogne.

 Refa Emmanuel Mwandemba aliyesaidiwa na Charles Simon na Kassim Mpanga aliwaonyesha kadi za njano mabeki Mghana Lamine Moro wa Yanga SC, Mganda Nico Wadada na mshambuliaji Muivory Coast, Richard Ella D’jodi wa Azam FC kwa makosa tofauti.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; David Kissu, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Daniel Amoah, Ally Niyonzima, Never Tigere, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Prince Dube/Richard Ella D’jodi dk23, Mudathir Yahya/Alan Thiery Akono dk51 na Ayoub Lyanga/ Idd Suleiman ‘Nado’ dk63.

Aidha, kikosi cha Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomary/ Said Juma ‘Makapu’ dk56, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Deus Kaseke/Faris Mussa dk70, Ditram Nchimbi/Michael Sarpong dk66 na Yacouba Sogne.

Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha alama 28 na kupanda kileleni, ikiwazidi  alama tatu Azam FC baada ya timu zote kucheza mechi 12  wakiwa mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye alama 23 za mechi 11.

Awali mechi nyingine za Ligi Kuu Ruvu Shooting imeichapa 1-0 Tanzania Prisons, bao pekee la Abrahman Mussa katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi mkoani Pwani.

Bao pekee la ushindi limepatikana dakika ya 30 na kuifanya timu ya Ruvu Shooting kusepa na pointi tatu mazima.

Mussa anafunga kwenye mechi mbili mfululizo ambazo ameanza kucheza kwenye kikosi chake bao lake la kwanza ilikuwa mbele ya Mbeya City, Uwanja wa Uhuru,Novemba 20.

Ushindi huo unaifanya Ruvu kufikisha jumla ya alama 22 ikiwa nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 12.

Wakati huo huo,Kagera Sugar imeichapa 3-0, mabao ya Erick Mwijage dakika ya 10, Nassor Kapama dakika ya 77 na Hassan Mwaterema dakika ya 79 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Nayo Gwambina FC ikaibuka na ushindi wa ugenini wa 4-3 dhidi ya jirani zao, Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Mabao ya Gwambina yamefungwa na Jimson Stephen dakika ya sita, Jacob Massawe dakkika ya 26 na 66 na Meshack Abraham dakika ya 45, wakati ya Mwadui FC yamefungwa na Herman Masenga dakika ya 15, Salum Chuni dakika ya 39 na Ismail Ally dakika ya 62.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news