Maafisa Mawasiliano Sekta ya Maji watakiwa kuwa wabunifu

Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji nchini wametakiwa kuwa wabunifu wanapotekeleza majukumu yao na kuhakikisha wanauhabarisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya sekta hiyo, anaripoti Happiness Shayo (WM).

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipokuwa akifunga kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji kilichomalizika leo mkoani Singida.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba (hayupo pichani) alipokuwa akifunga kikao hicho leo Novemba 6, 2020 mkoani Singida.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Maji, Bw. Florence Temba akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (kushoto) kufunga kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji kilichofanyika mkoani Singida.
 
“Ninatoa wito, muwe wabunifu, mwende na wakati, muandike makala katika vyombo vya habari na majarida na mutangaze Wizara kwa umma ikiwa katika taswira chanya,” Mhandisi Kemikimba amefafanua.

Mhandisi Kemikimba amewaasa Maafisa hao kutobweteka kwa kusubiria vyombo vya habari vitangaze kuhusu sekta hiyo kisha waanze kujibu hoja zilizotolewa na badala yake wahakikishe wanauhabarisha umma kwa wakati kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 inayowataka kutoa habari kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba (kushoto) akifunga kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji kilichofanyika mkoani Singida. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Maji, Bw. Florence Temba. Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA), Dkt. Mwidima Peter akichangia mada katika kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji kilichofanyika mkoani Singida.
 
Aidha, Mhandisi Kemikimba amewaagiza Maafisa Mawasiliano hao kuhakikisha wanaifahamu vyema sekta nzima ya maji kwa ukamillifu ili kutekeleza ipasavyo jukumu la kuitangaza vizuri taswira ya Sekta ya Maji.

Mhandisi Kemikimba alihitimisha kwa kuwataka Maafisa Mawasiliano kujitathmini kwa kuangalia endapo katika maeneo yao ya kazi wananchi wanapata huduma ya maji na kuangalia miradi inayotekelezwa katika maeneo hayo endapo inafanya kazi na kushauriana na watendaji wao namna bora ya kuitangaza miradi hiyo.
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA), Bi. Najibah Batenga akichangia mada katika kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji kilichofanyika mkoani Singida. 
 
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji baada ya kufunga kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Sekta ya Maji kilichofanyika mkoani Singida.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Masoko, Chuo cha Maji, Bi. Ghanima Chanzi amesema kikao kazi hicho kitamsaidia kuboresha utendaji kazi.

“Ujuzi huu utaniwezesha kuhakikisha jamii inatambua chuo cha Maji kinafanya majukumu gani ya msingi katika Sekta ya maji mathalani katika kuzalisha wataalamu wa sekta ya maji” Bi. Ghanima amesema.

Lengo la kikao hicho pamoja na masuala mengine ni kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi pamoja na kupata mafunzo juu ya masuala muhimu yanayohusu wajibu wa Maafisa Mawasiliano, Matumizi ya Mitandao ya kama njia ya Mawasiliano, Itifaki, Anuai za Jamii na umuhimu wa rasilimali za maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news