Machifu watakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuenzi mila na desturi za jamii

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bibi Leah Kihimbi ametoa wito kwa machifu nchini kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na kuzingatia kuwa mila na desturi imara ambazo ni msingi madhubuti wa kuendeleza jamii wanayoingoza na taifa kwa ujumla,
anaripoti Eleuteri Mangi, WHUSM-Dodoma.

Bibi Leah ameyasema hayo Novemba 11, 2020 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi katika hafla ya kusimikwa uchifu kwa Chifu Richard Luwawo wa Kata ya Matumbulu iliyopo jijini humo.
Akiongea na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Bibi Leah amewasisitiza machifu kutumia dhamana waliyopewa na wananchi kuhakikisha wanatunza, wanalinda na kuendeleza utamaduni wa mtanzania kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alivyosema, Taifa lisilo na utamaduni ni taifa mfu, hivyo ni wajibu wa kila mtanzania kuthamini utamaduni wa taifa. 

“Tanzania tuna utajiri mkubwa sana, tuna makabila zaidi ya 150, kupitia maafisa utamaduni waliopo katika kila halmashauri nchini ni wajibu wao kusaidia kutambua maeneo ambayo ni ya kihistoria na yanayotumika kwa matambiko, pamoja na kutoa elimu ya umuhimu wa kuhifadhi maeneo hayo alisema Leah. 

Naye Chifu Mkuu Kanda ya Kati Dodoma Henry Mazengo wa Pili wakati akimuapisha Chifu huyo alisema kuwa katika kutekeleza majukumu ya uongozi, machifu wanafanyakazi kwa kutumia mafiga matatu ambayo ni machifu, dini pamoja na Serikali ambayo yanafanyakazi kwa kushirikiana ikiwa ni pamoja na kukemea maovu, yanayokinzana na maadili ya kitanzania.

Aidha, Chifu Mazengo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuthamini mchango wa machifu nchini hatua inayowapa ujasiri wa kutekeleza majukumu vema.

“Rais ametuona sisi machifu na kurudisha cheo chetu ambacho tunakiona kama tunu ambayo ilipotea takriban miaka 40 iliyopita, Dkt. John Pombe Magufuli ni mtu mwenye maono ametuona sisi na kuturudisha katika nafasi yetu ya uchifu, tupo nyuma yake katika kutekeleza majukumu yetu na taifa litazidi kusonga mbele. 

Kwa upande wake Chifu Richard Luwawo wa Matumbulu ameahidi kuendeleza, kusimamia mila na desturi za eneo la utawala wake kwa kushirikiana na wananchi hatua itakayosaidia kuhakikisha mazingira yanatunzwa ili kutunza uasili wake ambayo ni chanzo cha mvua za kutosha kwa ajili ya shughuli za kwaletea maendeleo.

Naye Diwani wa Kata ya Matumbulu Emmanuel Chibago alisema kuwa katika kusimamia mila na desturi, wananchi wa kata ya Matumbulu wapo mstari wa mbele kwani wanatambua wajibu wao kukemea mienendo inayohatarisha maadili ya jamii yao kwa mila na desturi za Kigogo ambapo wazee huwakanya vijana hatua inayosaidia kuendeleza utamaduni wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news