Watu wanne wakazi wa Kijiji cha Kipilimka Kata ya Mwatundu Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega kwa tuhuma za makosa manane yanayohusiana na kumuozesha mtoto wa miaka 14, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Watuhumiwa hao wamesomewa makosa yao mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Rwekite na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iliyopo Wilaya ya Nzega.
Awali Mawakili hao wa serikali waliieleza mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega kuwa,mwezi Agosti kati ya tarehe 19 hadi 20, mwaka huu katika Kijiji cha Kipilimka Kata ya Mwatundu Wilaya ya Nzega mkoani Tabora watuhumiwa hao wakiwa ni wanne ambao ni Peter Zengo,Jumanae Zengo,Elizabet Richard na Modesta Mondesha wanakabiliwa na makosa manane ambayo baadhi yake ni kumuozesha binti mwenye miaka 14,kula njama ya kumuozesha,kushiriki ndoa isiyo halali na kujivika uhalisia usio wao.
Hata hivyo, watuhumiwa hao walikana mashitaka hayo na wapo nje kwa dhamana hadi Novemba 5, mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa tena.