Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora imemuhukumu, Meshack James (21) kifungo cha maisha jela ambaye anajishughulisha na kazi ya kusafirisha abiria kwa baiskeli mjini Tabora, anaripoti Mwandishi Diramakini.
James amehukumiwa baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka minne ambaye alipewa kazi na wazazi wa mtoto huyo ya kumpeleka shule na kumrejesha nyumbani mjini humo.
Imedaiwa mahakamani hapo na Wakili upande wa Jamhuri, Tito Mwakalinga kuwa, mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 154 Ibara ndogo ya kwanza na ya pili Julai 2, mwaka huu alipokuwa akimrudusha nyumbani mtoto huyo ambaye jina linahifadhiwa.
Katika maelezo hayo yaliyowasilishwa mahakamani na Wakili huyo katika shauri hilo la ukatili dhidi ya mtoto Namba 89/2020 likionesha madai ya kumlawiti mtoto huyo na kutolewa ushahidi na mashahidi watano.
Miongoni mwao ni daktari ambapo Mahakama imejiridhisha bila shaka kwamba kijana huyo alimfanyia ukatili huo wa kumlawiti mtoto huyo wa kiume akiwa nyumbani kwake na kisha kumtelekeza mtoto nje.
Aidha, Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, Jovin Kato ametoa hukumu hiyo akisema iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia chafu ambayo kimsingi haikubaliki katika jamii na kwamba inawadhalilisha watoto kwa ujumla ndani na nje ya mkoa huo.