Makamu mpya wa Pili wa Rais Zanzibar afunguka

Makamu wa Pili wa Rais Mteule wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah amesema wananchi wa Zanzibari wanapaswa kujenga matumaini makubwa kwa Serikali mpya itakayojizatiti kuwajibika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo.

Amesema, uwajibikaji huo utakaozingatia kutotoa nafasi kwa watendaji wenye tabia ya kukumbatia dhambi, ubadhirifu, uzembe pamoja na wizi ndio mfumo utakaotumiwa na Serikali chini ya usimamizi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah ametoa kauli hiyo akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kula kiapo cha Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Zanzibar na hapo hapo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid kulitamka jina lake lililowasilishwa na Rais wa Zanzibar mbele ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la kuteuliwa kwake kuwa Mtendaji Mkuu wa Serikali.

Amesema, viongozi, watendaji wa umma pamoja na wananchi lazima waelewe kwamba kasi ya upatikanaji wa huduma muhimu za msingi za kustawisha jamii na kukuwa kwa uchumi itategemea ushirikiano mkubwa utakaohusisha Serikali na wananchi.

Mheshimiwa Hemed amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kumuamini kumpa jukumu hilo zito ambalo amehaidi atalitekeleza kwa nguvu zake zote ili ile kiu ya Wazanzibari ya kuiona falsafa ya yajayo yanafurahisha iweze kufikiwa katika muda mfupi.

Makamu wa Pili wa Rais Mteule huyo wa Zanzibar amewathibitishia wananchi wote kwamba katika utekelezaji wake wa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Serikali hatakuwa tayari kuona Mtendaji aliyepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi anazembea katika nafasi yake.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla kabla ya uteuzi huo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Novemba 8, 2020 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba.
Moja ya sifa kuu ya Makamu wa Rais mteule ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla ni kuchapa kazi pia ana utamaduni wa kuwafikia wananchi kwa wakati kusikiliza na kuzifanyia kazi kero zao, pichani wakati akiwa Mkuu wa Mkoa akizungumza na wananchi na kuwafariji kutokana na kupata athari za mvua za masika katika Kijiji cha Mwambe ambapo zaidi ya nyumba 79  ziliezulia kutokana na upepo mkali hivi karibuni. Wachambuzi wa masuala ya siasa wameieleza Diramakini kuwa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amemteua mtu mwenye maono chanya ambaye anaweza kwenda na kasi yake ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa wakati. [Picha na MAKTABA].

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news