Amesema, Serikali Kuu kupitia Kamisheni yake ya Kukabiliana na Maafa licha ya jitihada kubwa inazoendelea kuchukua za kuona pale yanayotokea maafa inakabiliana nayo, lakini bado ipo haja ya kuona ushiriki wa wadau wote zikiwemo pia taasisi za ulinzi pamoja na wananchi unapatikana.Hayo ameyasema wakati akiwa kwenye ziara maalum ya kuzitembelea idara na taasisi zilizo chini ya ofisi yake ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ili kujitambulisha rasmi mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo lengo likiwa ni kuelewa mafanikio na changamoto zilizomp kwenye taasisi hizo.
Amesema, Taifa lazima lijipange kwa kuwa na wataalamu wake wa kutosha katika masuala ya kukabiliana na maafa kwa vile elimu ya masuala hayo kwa sasa inapatikana hapa nchini hadi ngazi ya shahada ya kwanza na matokeo ya faida yake yanaweza kuonekana ndani ya kipindi kifupi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka watendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa waendelee na uzalendo wao kwa kutekeleza majukumu waliyopewa na Taifa kwa vile yanawagusa moja kwa moja wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameelezea faraja yake kutokana na hatua kubwa iliyofikiwa kwa watendaji wa tume hiyo kuendelea kutoa elimu kwa umma mijini na vijijini na wakati mwingine hata kuvitumia vyombo vya habari katika kuifikisha taaluma hiyo kwa wananchi katika kukabiliana na maafa.