Makamu wa Pili wa Rais awataka wote kujitambua, kujitathimini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla amewaomba viongozi na watumishi wa umma wajitambue na kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao waliopewa na Taifa ili ile kiu ya kuwatumikia Wananchi ifanikiwe vyema, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Alisema baadhi ya Viongozi ama Watendaji watakaojihisi kwamba hawaendani na kasi ya Serikali iliyoanza kazi zake muda mfupi uliopita baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ni vyema wakaondoka kwa Heshima katika maeneo yao ya kazi waliyokabidhiwa.

Mhe. Hemed Suleiman Abdalla alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kupokewa ndani ya Ofisi yake Mpya kama Mtendaji Mkuu wa Serikali wakati akizungumza na Viongozi wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema hapendezi kuona baadhi ya Viongozi wa Taasisi na Wakuu wa Vitengo wanajifikiria maslahi yao binafsi hasa fursa za Masomo hata zile safari za nje ya Zanzibar zinazoambatana na masurufu bila ya kujali haki za Watendaji wao wa ngazi ya chini.

Aliwataka Watendaji hao wa Utumishi wa Umma wajisafishe kwa vile wao ndio wanaosimamia utendaji wa Serikali na kuacha malalamiko yasiyo na msingi kwani pale vinapojitokeza kikwazo katika uwajibikaji wao taratibu ziko wazi za kuwasilisha changamoto zao zinazowakabili katika ngazi ya juu.

Mheshimiwa Hemed Sueiman Abdalla aliwashukuru Viongozi Wakuu waliostaafu wa Serikali ya Awamu ya Saba Dr. Ali Mohamed Sheni na Balozi Seif Ali Iddi kwa ulezi wao mwema uliopelekea kumwajengea daraja ya pale walipofikia Viongozi wapya.

Aliwaomba Viongozi hao Wastaafu waendelee kuacha milango wazi kwa Viongozi Wapya ili pale watakapohitaji mawazo na busara zao katika uwajibikaji wa Utumishi wa Umma waweze kuitumia fursa hiyo adhimu.

Mapema akimkabidhi Ofisi pamoja na Nyenzo za Kazi Mtendaji Mkuu huyo Mpya wa Shughuli za Serikali Mh. Hemed Suleiman Abdalla, Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uteuzi wa Rais wa Zanzibar kumpa dhamana Mh. Hemed unatokana na ujemedari wake katika kusimamia maslahi ya Wananchi.

Balozi Seif alisema kwa umahiri wake Mheshimiwa Hemed Suleiman hana shaka na jukumu alilokabidhiwa la Umakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kuwaomba Viongozi na Watendaji wa Ofisi hiyo waendelee kumpa ushirikiano kama aliyopewa yeye wakati wa Utumishi wake.

Akitoa Taarifa ya makaribisho hayo ya Ofisi Katibu kuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed alisema kwa niaba ya Wafanyakazi wa Ofisi hiyo alimpongeza Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news