Mahakama ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma imemhukunu kwenda jela miaka miwili pamoja na faini ya shilingi milioni tano, Bi. Agnes Damian mwenye umri wa miaka 40 mkazi wa Mji Mwema Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Ni baada ya kupatikana na hatia ya kumkata na wembe sehemu mbalimbali za mwili binti wa miaka 15 ambaye ni mtoto wa mume wake, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Agnes amehukumiwa leo Novemba 30, 2020 na Hakimu, Eva Mushi wa mahakama hiyo.
Hakimu huyo amesema, adhabu hiyo inapaswa kuwa fundisho na onyo kwa wanaotenda matukio ya kikatili hasa kwa watoto ndani ya jamii.
Mama huyo anadaiwa kutenda tukio hilo Juni 18, mwaka huu ambapo aliingia chumbani na kufanya ukatili huo akimtuhumu kuwa Binti huyo alimpiga mtoto wake, hivyo lazima ampe onyo.
Kabla ya adhabu hiyo, Agnes ameiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa anatunza watoto wawili, ni yatima na hivi karibu amepona ugonjwa wa kupooza hajawa timamu kikamilifu.