Mashindano ya riadha, mbio za baiskeli kusherehekea Uhuru kufanyika Desemba 9,2020

Mashindano ya riadha na mbio za baiskeli ya kusherehekea Uhuru wa Tanzania yamepangwa kufanyika Desemba 9, 2020 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhuru Sports Agency, Leena Kapadia amesema kuwa, wanariadha wa kike na wa kiume watashindana kwenye mbio za nusu marathon kilomita 21 ambapo waendesha baiskeli watashindana mbio za kilomita 42.

Kapadia ameema kuwa, mbali ya mashindano hayo, pia kutakuwa na mashindano ya kilomita tano ya kukimbia au kutembea ambayo ni maalum kwa watu wazima, vijana na watoto na mbio za kilomita 10.
Amesema kuwa, usajili wa mashiriki katika mashindano hayo utaanza Novemba 15,2020 na kamati yao kwa sasa inatafuta wadhamini kwa ajili ya kufanikisha tukio hilo muhimu ambalo litakuwa la kwanza kufanyika nchini.

“Haya ni mashindano ya kwanza ya kusherehekea Uhuru wa Tanzania kwa kushirikisha wanariadha na waendesha baiskeli. Kampuni yetu imesajiliwa na Baraza la Michezo la Tanzania (BMT) na kupata namba ya usajili ya NSC 83 na tunatarajia kufanya mbio zenye mvuto na ushindani mkubwa,” amesema Kapadia.

Amesema kuwa, pia wanakusudia kuona viongozi mbalimbali, makampuni ya umma, binafsi, mabalozi, taasisi kushiriki katika mbio hizi.

“Mfano, mbio za kilomita tano ni maalum kwa viongozi mbalimbali, familia na watu mbalimbali, wote hawa wanatakiwa kusherehekea Uhuru wa nchi yetu, hivyo tunawaomba wanamichezo kujisajili kwa ajili ya kushiriki katika mashindano haya,”amesema.

Pia amesema kuwa, wanatarajia wanamichezo wasiopungua 3,500 kushiriki katika mashindano hayo ambapo miongoni mwao ni wanariadha nyota wa ndani ya nchi.

Kapadia amesema kuwa, mashindano hayo pia yana lengo la kuendeleza mchezo wa riadha na baiskeli hapa nchini. “Hii ni fursa ya wanamichezo kujipima uwezo wao kabla ya kuwania nafasi ya kufuzu mashindano mbalimbali ya kimataifa,”amesema Kapadia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news