Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu sita wilayani Ukerewe wakidaiwa kuchoma nyaraka mbalimbali za ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Kagunguli, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Amesema, watu sita bila kuwataja majina, wanashikiliwa na jeshi la polisi wilayani Ukerewe kwa tuhuma za kuvunja mlango wa jengo la ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kagunguli na kuchoma nyaraka mbalimbali za ofisi hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari.
“Watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kuchoma karatasi (nyaraka) mbalimbali kwenye ofisi hiyo ya Mtendaji wa Kata wakihisi kulikuwa na karatasi za ziada za kupigia kura,kabla ya kufanya tukio hilo walivunja mlango wa jengo hilo lenye ofisi sita,”amesema Muliro.
Amesema, jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika litawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewapongeza wadau wa uchaguzi mkoani humo kwa kufanya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu.
Muliro ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Amesema, katika Mkoa wa Mwanza,jeshi l polisi liliimarisha ulinzi na usalama kwa kiwango cha juu na kuufanya uchaguzi mkuu wa mwaka huu,kufanyika kwa haki, uhuru,amani na utulivu bila bughudha.
“Jeshi la polisi linawapongeza wadau wa uchaguzi ambo walitoa taarifa mbalimbali za watu waliokuwa wakipanga njama za kufanya vurugu na fujo ambo walikamatwa na kuhojiwa baadaye kuachiwa kwa dhamana na kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani,hakuna matukio makubwa ya ajabu ya kuathiri mchakato wa uchaguzi mkuu,”amesema Muliro.
Tags
Mahakamani