Miezi 24 ijayo Butiama, Musoma kufurika maji safi na salama

Wizara ya Maji imesaini mkataba na Mkandarasi wa ujenzi wa mradi mkubwa wa Maji wa Mugango- Kiabakari UNICK CONSTRUCTION ENGINEERING (LESOTHO) ( PTY) LTD. He Yifeng / Paul He utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 70.5 ambapo utaweza kuhudumia wananchi zaidi ya 200,000 wa vijiji 19 kutoka Wilaya ya Butiama na Musoma Mkoa wa Mara na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 24,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Leo Novemba 17, 2020 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandidi Anthony Sanga ameongoza zoezi la utiaji saini kwa pamoja na Mkandarasi wa kampuni hiyo hafla ambayo imefanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mjini Musoma.

Hafla hiyo imehudhuriwa na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Maji na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, ambapo pamoja na mambo mengine Sanga amemtaka Mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili umalizike kwa wakati waananchi waanze kunufaika na mradi huo.

"Niombe Mkandarasi unayejenga mradi huu uukamilishe kwa wakati, fanya kazi usiku na mchana wananchi wa maeneo husika wanahitaji sana huduma ya maji safi na salama.

"Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli katika ahadi yake alipokuja Mkoa wa Mara kuomba kura alisema akichaguliwa tu lazima kazi ianze na ameanza kutekeleza, itakuwa ni ajabu kuona Mkandarasi unasua sua na kushindwa kuukamilisha kwa muda uliopangwa kwenye mkataba wakati fedha zipo tena zimetolewa kutoka Badea na Saud Fund,"amesema Katibu Mkuu huyo.

Ameongeza kuwa, mradi huo ukikamilika utaweza kutoa huduma ya maji kwa wananchi kwa miaka 20 kwa utoshelevu, ambapo pia utazalisha lita zaidi ya milioni 17 awamu ya kwanza kwa siku, huku uhitaji ukiwa ni lita milioni 12 kwa siku na awamu ya pili utazalisha lita zaidi ya milioni 35 na baadhi ya vijiji vitaongezwa kwenye mradi na akasisitiza Mkandarasi kuzingatia ubora wa mradi, muda wa kukamilika na thamani ya fedha zinazojenga mradi huo.

Mhandisi Sanga amemtaka Mkandarasi huyo kuwapa nafasi za kazi wananchi waliopo maeneo ya mradi ili waweze kuwajibika kuchimba mitaro na kazi nyingine zisizo za kitaalamu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwafanya wajipatie kipato kipindi chote cha mradi huo.

Sambamba na viongozi wa maeneo husika wakitakiwa kutoa ushirikiano kwa mkandarasi kipindi chote cha mradi huo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye baadhi ya vijiji vya jimbo lake vitanufaika na mradi huo, Jumanne Sagini, amesema wakazi wa Butiama wataondokana na adha ya maji inayowakabili kwa sasa baada ya mradi kukamilika.

"Ilikuwa ni aibu sana maji yanaenda mbali zaidi ya kilomita 400 mikoa ya mbali, lakini wananchi wa Butiama na Musoma wanakosa maji wakati wanazungukwa na Ziwa Victoria, nimshukuru sana Rais kwa uamuzi wake wa kuleta mradi huu haraka iwezekanavyo baada ya kuapishwa, hakika amejibu ombi na kilio cha wananchi, niombe pia kata zinazopakana na Mto Mara ikiwemo Kata ya Buswahili na Bukabwa ikiwezekana ziangaliwe nazo ziwekwe kwenye mradi awamu nyingine. Wananchi wapelekewe huduma ya maji,"amesema Mbunge huyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Butiama Annarose Nyamubi amesema kuwa, atahakikisha anahusisha watendaji wa vijiji I'll kulinda miundombinu ya mradi huo huku akikiri kuwa tatizo la maji ni kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo akiwemo yeye.

Mkuu huyo amesema tangu awe Mkuu wa wilaya hiyo anakabiliwa na ukosefu wa maji na wakati akiwa Mkuu wa Wilaya katika Mkoa wa Shinyanga iliyo mbali na Ziwa Victoria, alikuwa akipata maji muda wote.

Mkandarasi anayejenga mradi huo, UNICK CONSTRUCTION ENGINEERING (LESOTHO) (PTY) LTD, He Yifeng/ Paul He amesema kuwa atahakikisha anafanya kazi usiku na mchana aweze kukamilisha mradi huo kabla ya muda wa miezi 24.

Pia amesema anatambua dhamana aliyopewa ni kubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa ajili ya maendeleo yao.

Aidha, wakati wa kampeni Mgombea Ubunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo aliwahakikishia wananchi wa jimbo hilo kuwa, iwapo watakichagua chama hicho kama walivyofanya Oktoba 28, mwaka huu, watarajie mambo mazuri kutoka Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutokana na dhamira thabiti ya kuleta maendeleo kwa wananchi na neema nyingi kama ilivyoainishwa kwenye ilani yake ya uchaguzi.

Awali akitoa taarifa fupi ya mradi uliopo kwa sasa unaohudumia wananchi, Mkurugenzi wa Mamalaka ya Maji Mugango - Kiabakari,Mhandisi Cosmas Sanda amesema mradi uliopo umechakaa sana wakati ukianza mwaka 1974 ulikusudiwa kuhudumia watu 300,000. 

Ambapo kwa sasa unahudumia watu 165,000 pekee na maji yanayopotea kutokana na kuchakaa kwa miundombinu ni asilimia 76, huku asilimia 24 pekee ndiyo wanasambaza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news