Mwalimu Makuru awapa somo wanasiasa asisitiza uzalendo

Viongozi wa vyama vya siasa nchini wameaswa kutanguliza mbele uzalendo kwa Taifa na hivyo wamehimizwa kuiunga mkono Serikali iliyochaguliwa na wananchi katika kuhakikisha shughuli za maendeleo zinazidi kufanyika nchini, anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini), Mara.
Mwalimu Makuru Lameck Joseph. (DIRAMAKINI).
Wameombwa kuweka mbele maslahi ya Taifa na kuondokana na tabia ya kuhamasisha wananchi kuichukia Serikali ama kutoipa ushirikiano, badala yake wametakiwa kuachana na chuki na kushikamana na Serikali na wananchi kwa dhati katika kuhakikisha kwamba nchi inazidi kusonga mbele kimaendeleo.
 
Mwalimu Makuru Lameck Joseph ameyasema hayo leo Novemba 17, 2020 mjini hapa huku  akiwapongeza watanzania kwa kutimiza haki na wajibu wao wa kikatiba wa kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu kwa uhuru na haki.

"Niwaombe viongozi wa vyama vya siasa vyote washikamane na serikali, huu sio muda wa kufanya malumbano huu ni muda wa kuchapa kazi kuimarisha maendeleo ya Taifa letu, uchaguzi ulimalizika, kwa hiyo ni jukumu letu sote kushiriki katika maendeleo na kuweka kando maslahi ya vyama, tuweke mbele maslahi mapana ya Watanzania wote bila kujali vyama vyao,"amesema Mwalimu Makuru.
 
Mwalimu Makuru ameviasa vyama vya siasa ambavyo vimepata wabunge wa viti maalumu kutokana na kukidhi asilimia zilizowekwa kwa mujibu wa sheria, kutowazuia kwenda bungeni kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi waliopiga kura, akasisitiza wawaruhusu wabunge wake wakatimize wajibu wao wa kutoa michango mbalimbali bungeni kwa maslahi ya Watanzania wote.

Katika hatua nyingine, Mwalimu Makuru Lameck amewaasa Watanzania wote kuendelea kuchapa kazi halali za maendeleo kwa bidii ikiwa ni utekelezaji wa kauli mbiu ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu huku pia akiwashauri viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza kumtanguliza mbele Mungu katika kazi zao ili awawezeshe wingi wa hekima, busara na maarifa wanapowatumikia wananchi kutatua kero zao.

"Tuna wajibu wa kuendelea kuiombea nchi yetu na viongozi wote, mahali ilipo kwa sasa ni pazuri sana nchi imepiga hatua kiuchumi na katika kuongeza huduma za kijamii kwa wingi, Watanzania watarajie mambo mengine makubwa yatafanyika ndani ya miaka mitano ijayo cha msingi ni kuiamini Serikali na kuipa ushirikiano wa dhati,"amesema Makuru aliyekuwa miongoni mwa watia nia wa Ubunge Jimbo la Musoma Mjini mkoani Mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news