Serikali kwa kutambua kero ya upatikanaji wa majisafi na salama
inayowakabili wananchi wa Ilemela hususan Kata ya Buswelu imeamua
kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 5.1 ili kuondokana na adha hiyo,
anaripoti Mohamed Saif, Mwanza.
Hayo yamebainika Novemba 19, 2020
wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika na
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mkoani Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele iliyolenga kukagua
ujenzi wa tenki la maji la lita milioni tatu linalojengwa kwenye kata hiyo.
Dkt. Lalika amesema, mradi huo wa tenki ni miongoni mwa miradi
ambayo ilitengewa fedha mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni utekelezaji wa
sera ya Serikali ya kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu
kufuata huduma ya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele wakikagua ujenzi wa mradi wa maji unaojengwa kwenye Kata ya Buswelu. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji unaojengwa kwenye Kata ya Buswelu.
“Serikali ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli ilijipambanua
vyema kutetea wananchi wake na kwamba mwananchi hapaswi kutembea zaidi
ya mita 400 kufuatilia huduma ya maji,” amesema Dkt. Lalila.
Amefafanua
kwamba, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mwananchi anapata muda mwingi
wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo ili kujiongezea kipato na
hivyo kukuza uchumi wake binafsi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Amesema,
anatambua miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na MWAUWASA kwenye
wilaya hiyo na aliipongeza kwa jitihada zake katika kusimamia ujenzi wa
miradi ya maji kwa niaba ya Serikali ambapo alisema kupitia miradi hiyo
kero ya maji inakwenda kuwa historia. Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika akipata maelezo ya ujenzi wa tenki la lita milioni tatu linalojengwa wilayani humo kutoka kwa Mtaalam Mshauri, Mhandisi Andrew Seleli.
Hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa tenki la maji la lita milioni tatu linalojengwa kwenye Kata ya Buswelu Wilayani Ilemela.
“Natambua MWAUWASA inatekeleza miradi mingine ya maji Wilayani Ilemela
mbali na huu tuliotembelea leo ambayo ni pamoja na Mjimwema, Nyasaka,
Nyamhongolo, Kabusungu, Kabangaja, Igalagala na Kayenze, ninaamini kero
ya maji itabaki historia,” amesema Dkt. Lalika.
Akizungumzia
utekelezaji wa mradi, Mhandisi Msenyele alisema unagharamiwa na Serikali
kwa asilimia Miamoja kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa
wahisani ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la
Maendeleo la Ufaransa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa tenki la maji kwenye Kata ya Buswelu. Anayemfuatia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele.
Amesema, ujenzi wa tenki hilo ulianza rasmi Septemba, 2020 na kwamba unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Julai 2021.
“Shughuli tunazoendelea nazo hivi sasa ni kuandaa umwagaji wa zege ya awali ya kuandaa kitako cha tanki, kutengeneza barabara ya kuelekea kwenye tenki pamoja na maandalizi ya umwagaji zege za kuta za tenki,” alisema Mhandisi Msenyele.
Amefafanua kwamba, mradi unahusisha ujenzi wa tenki la lita milioni tatu, ulazaji wa bomba urefu wa kilomita 14 na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kufika kwenye tenki ambacho kinajengwa kwenye eneo la Kiseke Jeshini.
Amebainisha kwamba, kukamilika kwa mradi huo wa tenki kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba, Kahama, Bujigwa, Nyamadoke na Ilalila.
Mhandisi Msenyele amesema, mradi huo ni sehemu ya Programu ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza (LV WATSAN) na kwamba unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).