Kaa mbali na wanafunzi, ipo hivi Mwenyekiti wa Kijiji cha Ijinga Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza, Badri Juma Masengo (40) anadaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita wa Shule ya Msingi Ijinga mwenye umri wa miaka 15 jina tunalo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Magu limechukua hatua za haraka na linamshikilia mwenyekiti huyo kwa mahojiano akituhumiwa kutenda kosa hilo kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli amesema hakubaliani na hatakubali kuona watoto wa kike wanakatishwa masomo na wanaume wenye uchungu wa ngono wanaohangaika na wanafunzi wakati wanawake wamejazana mitaani na kuonya wenye tabia hiyo na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
DC huyo amesema, katika wilaya hiyo yapo mambo ya ovyo yanafanywa na baadhi ya walimu, wazazi na jamii kwa kufanya ngono na wanafunzi wa shule na kukatisha ndoto zao za elimu na kuonya hatakubali hayo yaendelee huku akitoa angalizo kwa watumishi wa idara ya polisi na mahakama wanaopindisha sheria sababu ya rushwa kwenye kadhia hiyo hawatabaki salama.
Amesema kuwa, Rais Dkt. John Magufuli amefuta ada kwa shule za msingi hadi kidato cha nne na kurahisha mambo kwa wananchi ambao hawakuwa na uwezo ili kuwawezesha watoto kusoma kwa raha watimize ndoto zao, lakini watu wachache kwa tamaa ya ngono wanawaharibia maisha.
“Ilani ya uchaguzi Ibara ya 80 inaeleza uboreshaji wa elimu kutoka msingi hadi chuo kikuu mtoto asome hadi mwisho hata kama mzazi hana uwezo na serikali inataka wasome kwa raha watimize ndoto zao na hivyo sitawavumilia wanaume wanaojamiana na watoto na nitoe rai kwa idara ya mahakama na polisi watende haki kwa mtoto aliyekatishwa masomo na mwenyekiti huyo ili liwe fundisho kwa wengine wanaokiuka maadili na kuharibu maisha ya watoto,”amesema.
Mkuu huyo wa wilaya amesema tatizo la rushwa kwa baadhi ya watumishi wa mahakama na polisi wasio na uadilifu,linakwamisha juhudi za serikali na kuwataka kuzingatia kauli ya Rais Magufuli wakati akimwapisha Mwanasheria Mkuu.
“Jaji Mkuu wa Tanzania naye alirudia maneno hayo,na mimi leo naelekeza sina shaka na sitaki kuamini kuwa rushwa itatembea kwenye kesi hii,sitaki kuhukumu maana ushahidi uko wazi, hivi mpepelezi katika kesi hii anataka kueleza nini na ninaomba isichukue muda mrefu ili haki itendeke,”amesema Kalli.
Mwanafunzi huyo mwenye ujauzito wa wiki 11 miezi miwili na wiki moja alisema, kwa muda mrefu mtuhumiwa huyo Badri Juma alikuwa akimtongoza ambapo alimfuata nyumbani kwao majira ya saa 6 usiku baada ya wazazi wake kwenda msibani na kumwacha na wadogo zake na kumshawishi kuondoka naye hadi kwake.
Amesema, walipofika nyumbani hapo mtuhumiwa huyo alimvua nguo kisha akampatia sh. 20,000 na kumwingilia,hata hivyo baada ya kutimiza haja zake alimnyang’anya fedha hizo na kumrejesha tena kwao usiku huo huku akimpa ahadi ya kumpa matumizi na nguo, lakini hakutimiza ahadi hiyo.
Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Magu, Glory Vicent Mtui amempongeza mkuu wa wilaya hiyo kwa jinsi anavyoshughulikia changamoto ya mimba kuhakikisha wahusika wanakamtwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuahidi hawatafumbia macho suala la mwanafunzi huyo licha ya baadhi ya wazazi kuwaficha wahalifu kwa kupewa rushwa sababu ya mazingira magumu na umasikini.
"Tangu Januari, mwaka huu takwimu za mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi ni 28 na siamini mzazi yeyote anafurahia mwanaye kukatishwa masomo na hili tatizo la mimba tutafanya kazi ya kukabiliana nalo na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani na hadi sasa zipo kesi 28 baadhi ziko mahakamani na zingine watuhumiwa wamekimbia ama kuachiwa sababu ya changamoto ya rushwa kwa mashahidi,”amesema Mtui.
Afisa Mtendaji wa Kata Kahangara, John Clavery Mabati amesema kuwa, mtuhumiwa alipokamatwa na kuhojiwa alikiri kufanya ngono na kumpa ujauzito mwanafunzi huyo na ili kujinasua na mkono wa sheria alijaribu kumshawishi kwa kumpa rushwa ya sh.milioni mbili akaikataa.
Amedai, kabla watu waliotumwa kumkamata mtuhumiwa huyo walihongwa kabla ya kumkamata Novemba 4, mwaka huu ambapo alimfahamisha DC (Mkuu wa Wilaya) naye akaagiza asiachiwe ndipo wakamfikisha polisi kwa hatua za kisheria.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ijinga, Ncheyeki Casmir amesema, mwanafunzi huyo ambaye alikuwa miongoni mwa 10 waliopelekwa kwenye vipimo vya mimba,alibainika kuwa na ujauzito na hakuwahi kuwaeleza wazazi kitendo alichofanyiwa.
Amesema, walipomhoji mwanafunzi huyo aliwaeleza kila kitu kuhusu suala hilo na kwamba siku wazazi wake wakiwa wamekwenda kulala msibani usiku mtuhumiwa alifika nyumbani kwao akamshawishi na kumchukua usiku huo na kwenda naye nyumbani kwake na kumwingilia huku akimpa ahadi ya kumhudumia.
Naye mama mzazi (jina linahifadhiwa) wa mwanafunzi huyo amesema, licha ya kuwa wanalala nyumba moja na binti yake hakuwahi kumweleza lolote kuhusu Badri na alipata taarifa ya ujauzito kutoka kwa walimu baada ya kuitwa shuleni na kuelezwa juu ya hali hiyo.
Kitendo hicho kiovu kilichotendwa na Mwenyekiti huyo ni sawa na kumjaribu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Magufuli ambaye mara kwa mara amekuwa akikemea vitendo vya namna hii kwa wanafunzi kutendewa kwani wanaharibiwa ndoto zao.
Mwandishi Diramakini anakupitisha katika maonyo ya Rais kwa nyakati tofauti mwaka jana hususani mkoani Rukwa;
Rais Dkt. Magufuli akiwa zirani mkoani Rukwa mwaka jana alishangazwa na kutokuchukuliwa hatua dhidi ya wanaume wanaotuhumiwa kuwapachika mimba wanafunzi 229 mkoani Rukwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
"Serikali inatoa mchango kwa kutoa elimu bure na wanaume bure wanawapa mimba watoto wa shule! Hao wanaume bure 229 ndio viongozi? Kwa sababu kama sio hao viongozi, je viongozi wameshindwa kitu gani kuwapeleka hawa watoto kwenye haki?
"Watoto 229 wamekatiliwa maisha yao katika elimu," alisema Rais Magufuli huku akiwataka viongozi wa serikali pamoja na wa kidini mkoani humo kulivalia njuga tatizo hilo haraka. Agizo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi nchini kote ili kuwapa haki wanafunzi wote kusoma bila kukatizwa na mafataki.
Pia Rais Magufuli aliwasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa na malengo madhubuti ya kesho yao.
"Lengo la serikali ni wanafunzi wote wasome bure kuanzia shule ya msingi, sekondari na matarajio ni mpaka chuo kikuu. Ukiambiwa wewe mzuri mwambie akamwambie mama yake, msiogope kuwapa maneno magumu, nataka msome, nyinyi ndio marais wa kesho, mawaziri na wabunge."Nia ya serikali yangu ni kuleta maendeleo, kila mmoja awe tajiri, watoto someni....alisema huku akiendelea kutoa maonyo kuwa;
"Tuwaogope mabinti zetu na tuwalee binti zetu na tusiwadanganye kwa fedha tunazopata, maana wanaume wanaofanya hayo mambo ni wanaume wakubwa tu na inawezekana hata wana wake wawili nyumbani na hawajawahi kuwanunulia hata nguo na bado wanawakimbilia watoto wadogo wa shule...
"Hata kama mwalimu wako anakwambia anakupenda penda mwambie hayohayo majibu, takwimu za mimba mkoa huu zinatisha. Nilitegemea wanaume 229 wawe wamefungwa ila mpaka sasa sina hakika kuwa hata mmoja amefungwa".
"Viongozi wa mkoa na wilaya mbalimbali, hii ni aibu. Kwenye kata yako diwani awepo na watoto wamepata mimba basi wewe hutoshi. Viongozi wa dini inabidi tukemee jambo hili kwa nguvu zote, hili linatupa doa katika taifa leo," alisisitiza.
hii maakala nzuri snaaaa jamii inapaswa kujifunza
ReplyDelete