Nabii Joshua atabiri miaka mitano ya maendeleo ya kihistoria Tanzania, awapongeza Rais Magufuli, Mwinyi

Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala amesema, ushindi mkubwa walioupata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi ni ishara kwamba Watanzania wana imani kubwa na 
viongozi hao.Pia Mungu amemuonyesha kuwa, kupitia viongozi hao ndani ya miaka mitano ijayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda kuandikisha miradi na maendeleo ya kihistoria, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala. (Diramakini).

Nabii Joshua ameyasema hayo leo Novemba 5, 200 jijini Dodoma muda mfupi baada ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

"Awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufanya Uchaguzi Mkuu kwa utulivu na amani. Hali ambayo imedhihirisha kuwa, Watanzania wana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi ili kupata watu sahihi watakaowezesha kuharakisha maendeleo.

"Maamuzi yao sahihi ambayo yanatokana kabisa na maombi mfululizo ambayo tulikuwa tunayaomba sisi watumishi wa Mungu yamewezesha kupata viongozi makini na sahihi kwa ajili ya kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kila mara ninaposimama katika maombi, Mungu amekuwa akinionyesha kuna jambo ameliweka kwa Mheshimiwa Dkt.Magufuli na Mheshimiwa Dkt.Mwinyi kwa ajili ya Watanzania, hivyo tuendelee kuwaombea na kufanya kazi kwa bidii, tutashuhudia mafanikio makubwa," amesema Nabii Joshua.

Amesema, miongoni mwa mambo ambayo Mungu amekuwa akimuonyeshwa kutoka kwa Rais Dkt. Magufuli na Rais Dkt. Mwinyi ni pamoja na uwezekano wa kuivusha Tanzania kutoka uchumi wa kati ndani ya miaka michache ijayo kwenda katika uchumi wa juu.

Nabii Joshua amesema, viongozi hao wawili wana hofu kubwa ya Mungu ndiyo maana kila mara rais Dkt.Magufuli amekuwa akisisitiza kila jambo Watanzania wamtangulize Mungu, jambo ambalo ni la baraka zaidi katika Taifa la Tanzania.

Pia amesema, Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yenye makao yake makuu Yespa mjini Kihonda, Morogoro itaendelea na Programu ya Kuliombea Taifa, hiyo ikiwa ni kampeni endelevu kwa ajili ya kuwaleta Watanzania pamoja ili waweze kumtanguliza Mungu mbele katika kila jambo ambalo wanataka kulitekekeza. 

Hatua ambayo itawezesha kila mmoja kumtumainia Mungu kwa kila jambo ambalo analitekeleza, kwa mustakabali wa umoja na mshikamano wa wao na Taifa kwa ujumla.

"Mfano nikitoka hapa, ninaelekea katika maombi, ikiwa ni utaratibu wa kufanya maombi mfululizo kwa ajili ya kuliombea Taifa, viongozi na Watanzania wote. Ninaamini kupitia maombi, Taifa la Tanzania litazidi kuwa na amani ya kudumu ambayo itapigiwa mfano kila siku na mataifa iwe madogo au makubwa duniani, hivyo ni wajibu wetu Watanzania kuendelea kuliombea Taifa letu bila kuchoka,"amefafanua Nabii Joshua.

Rais Dkt. Magufuli ameapishwa leo Novemba 5, 2020 jijini Dodoma baada ya kuibuka mshindi kwa kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali zilizopigwa kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu huku Tundu Lissu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,933,271 ya kura zote zilizopigwa.

Matokeo hayo yakiwa ni kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huku kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Rais Dkt.Hussein Mwinyi wa CCM akiibuka mshindi kwa kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 akifuatiwa na Maalim Seif Sharrif Hamad wa Chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 96,103 sawa na asilimia 19.87.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news