Leo Novemba 1, 2020 Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) imekabidhi vyeti vya ushindi kwa kiti cha Rais kwa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan baada ya kuibuka kidedea kwa asilimia 84.4 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Dkt.Magufuli akizungumza katika viwanja vya NEC Njedengwa jijini Dodoma muda mfupi mara baada ya kukabidhiwa cheti hicho amewashukuru watanzania kwa kumuamini huku akisema wamempa deni na ameahidi kufanya kazi mchana na usiku ili kuwatimizia mahitaji yao katika kuwaletea maendeleo katika miaka mingine mitano ijayo.
Amesema, ushindi wa kishindo kwake, wabunge na madiwani ni deni kubwa kwa Watanzania wote, " namuomba Mwenyezi Mungu anisaidie katika awamu hii tuweze kutimiza haja ya watanzania waliotuamini,kupata asilimia 84.4 ni imani kubwa. Imani hiyo nitatumia kwa kufanya kazi usiku na mchana," amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akionesha Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Urais alichokabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage mara baada ya kutangazwa mshindi kwa Kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
"Leo nimepokea cheti cha ushindi wa nafasi ya Urais baada ya Watanzania kutupigia kura za kutosha, mimi na Mgombea wa Makamu Samia suluhu, katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020.Mimi na Mama Samia Suluhu tunawashukuru kwa imani mliyotuonesha kwa kutupatia ushindi mkubwa wa 84.4%, mmetuachia deni kubwa la kuwatumikia, na tunawaahidi utumishi wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa letu,"amesema Dkt.Magufuli.
Tags
Habari