NECTA yatangaza shule 10 bora Matokeo Darasa la Saba 2020

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limeitangaza Shule ya Msingi God’s Bridge kuwa ndiyo shule bora kitaifa baada ya kushika nafasi ya kwanza, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Matokeo hayo yametangazwa leo Jumamosi, Novemba 21, 2020 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Charles Msonde.

Kwa mujibu wa NECTA,shule hiyo iliyopo mkoani Mbeya imeipiku Shule ya Msingi Graiyaki ya mkoani Mara iliyokuwa imeshika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani ya darasa la saba mwaka 2019. Katika matokeo ya mwaka huu Graiyaki imeporomoka hadi nafasi ya tano.

God’s Brigde, ambayo haikuwepo katika shule 10 bora mwaka jana, katika matokeo ya mwaka huu imefuatiwa kwa karibu na Bunazi Green Acres ya mkoani Kagera pamoja na Twibhoki ambayo imeendelea kung’ang’ania katika orodha hiyo ya juu.

Shule nyingine zilizofanikiwa kuingia kwenye 10 bora katika matokeo ya mwaka 2020 yaliyotangazwa leo ni Kwema Modern ya Shinyanga, Kemebos na Rweikiza za Kagera, St Anne Marie (Dar es Salaam), Mumtaaz (Mwanza) na Rocken Hill ya Shinyanga.

​Kati ya shule 10 zilizoingia katika orodha hiyo nane zinatokea Kanda ya Ziwa na kuifanya kanda hiyo kuendelea kutawala katika matokeo hayo ya darasa la saba.

Shule tisa kati ya 10 zilizotangazwa katika 10 bora zilikuwa na madarasa yenye wanafunzi wasiozidi 100 kasoro Shule ya St Anne Marie pekee iliyokuwa na wanafunzi 129 ambao ni takriban mara tatu ya wanafunzi waliokuwepo God’s Bridge.

Shule hiyo ya God’s Bridge iliyoongoza kitaifa ilikuwa na wanafunzi 47 pekee kwa mujibu wa NECTA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news