Timu ya Taifa ya Tanzania, chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes leo Novemba 22, 2020 imeibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Djibouti kwenye mchezo wa Michuano ya CECAFA uliochezwa Uwanja wa Black Rhino Academy uliopo wilayani Karatu jijini Arusha. Ni katika mchezo wa Kundi A michuano ya CECAFA U20, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtanange huo wa nguvu, Abdorahman Kamil dakika ya 14 wa Djibouti alianza kupachika bao la kwanza ambalo lilidumu mpaka mapumziko na kuwafanya Ngorongoro Heroes kwenda kutafuta mbinu mpya kupata ushindi.
Chini ya Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jamhuri Khwelo (Julio) mambo yalibadilika dakika saba mbele baada ya kipindi cha pili kuanza baada ya Teps Theonasy kupachika bao la kwanza dakika ya 52.
Mabao mengine yalifungwa na Abdul Hamis ambaye mabao yake alifunga dakika ya 63,72 na 90 kwa mkwaju wa penalti.
Aidha, Khelfin Hamdoum naye alikuwa miongoni mwa watupiaji alifunga bao dakika ya 82 pamoja na Andason Kimweli kwenye mchezo wa ufunguzi uliokuwa na ushindani mkubwa.
Michuano hii ambayo Tanzania ni wenyeji inashirikisha timu tisa ambazo ni pamoja na Kenya, Sudan, Uganda, Sudan Kusini, Somali, Djibouti, Ethiopia,Burundi na wenyeji ambao ni Tanzania.