Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20 ya Ngorongoro Heroes, Jamhuri Kihwelo (Julio) ameendelea kutabasamu, baada ya vijana wake kuendelea kufanya maajabu uwanjani, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Awali amesema kuwa, wanaamini watapata ushindi mbele ya Somalia kwenye mchezo wa pili wa mashindano ya CECAFA na hatimaye vijan wamewezesha ushindi mnono wa goli nane kwa moja.
Kwenye mchezo huo wa Kundi A michuano ya CECAFA U20 Novemba 26, 2020 katika Uwanja wa Black Rhino Academy uliopo Karatu mkoani Arusha, Tanzania walionekana kuutawala zaidi mchezo huo.
Mabao ya Ngorongoro Heroes yamefungwa na Hamisi Suleiman dakika ya tatu, Ben Starkie dakika ya 14, Kelvin John 'Mbappe' dakika ya 28, 33 na 55, Kassim Haruna dakika ya 47, Frank George dakika ya 65 na Anuary Jabir dakika ya 86, wakati la Somalia limefungwa na Sahal Muhumed dakika ya sita.
Kwa ushindi huo, Tanzania inafikisha alama sita na kuongoza Kundi A ikitinga Nusu Fainali ambako itakutana na Mshindi wa Pili Bora baina ya makundi yote Jumatatu ijayo.
Ngorongoro Heroes kwenye mchezo wao wa ufunguzi uliochezwa Novemba 22, dhidi ya Djibouti, waliibuka na ushindi wa mabao 6-1 huku Abdul Hamis akiweka rekodi ya kufunga hat trick na kuondoka na mpira wake kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Black Rhino Academy mjini Karatu.