Ni pambano la kufunga mwaka kati ya Mwakinyo na Paz Novemba 13

Rais wa Chama cha Ngumi za Kulipwa (WBF), Howard Goldberg atawasili nchini Jumatano kwa ajili ya usimamizi wa pambano la ubingwa wa mabara Super-Welter Weight kati ya bondia, Hassan Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina linalotarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oysterbay jijini Dar es Salaam Ijumaa ya Novemba 13,2020.
Mbabe wa ngumi, Hassan Mwakinyo anahitaji maombi ya Watanzania akafanye kweli. (MAKTABA/Diramakini).

Goldberg atawasili pamoja na mwamuzi wapambano hilo, Edward John Marshall saa 3.15 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya, KQ.

Mbali ya kuwa Rais wa WBF, Goldberg enzi zake alikuwa mwamuzi na jaji wa ngumi za kulipwa duniani akiwa amecheza zaidi ya mapambano 300 katika nchi mbalimbali.

Goldberg anakuja nchini kwa mara ya sita kwa ajili ya kusimamia ngumi za kulipwa na amefurahishwa sana na weledi wa kampuni ya Jackson Group Sports katika pambano hili kwani wamekwisha kamilisha masharti yote ikiwa ni pamoja na tiketi za ndege za ujio wao.

Amesema kuwa, kampuni ya Jackson Group Sports imeonyesha njia chanya katika kuandaa mapambano ya ngumi za kulipwa kwa weledi na uwazi mkubwa, jambo ambalo limewafanya wao kutoa kibali na kuja kusimamia pambano la Mwakinyo dhidi ya Paz.

Amesema kuwa, kila kitu ambacho WBF ilikihitaji kutoka kwa waandaaji wa pambano hilo kilipatikana na kukamilishwa haraka, jambo ambalo limewapa faraja kubwa.

Kwa mujibu wa Goldberg, ujio wa Jackson Group Sports kwenye ngumi ni fursa kwa mabondia wenye lengo la kupata maendeleo na anaamini Tanzania kupitia Jackson Group Sports itapata mabondia wengi wenye vipaji.

Amesema kuwa, ametembelea nchi zaidi ya 60 duniani kwa kazi kusimamia mapambano ya WBF, lakini amekuwa na furaha zaidi kuja Tanzania yenye vivutio vikubwa vya utalii ikiwa no pamoja na Hifadhi ya Serengeti na Zanzibar.

“Nimekuwa nikiulizwa na baadhi ya maafisa wa WBF kwa nini napenda kuja Tanzania, jibu ni rahisi sana, ni nchi yenye uzuri wa asili na vivutio vingi vya utalii, wananchi wake wana upendo mkubwa na ushirikiano ambao nimekuwa nikiupata na serikali kupitia Wizara ya Michezo na mapromota,” amesema Golberg.

Wakati huo huo mabondia Fatuma Zarika atawasili nchini kwa ajili ya pambano lake dhidi ya Patience Mastara wa Zimbabwe ambaye atawasili Jumanne usiku.

Mkurugenzi wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema kuwa, Zarika atawasili saa 3.30 usiku tayari kwa pambano hilo. Tayari Mpinzani wa bondia Hassan Mwakinyo, Paz amewasili nchini na anaendelea kujifua.

Amesema kuwa, mabondia wengine, Alex Kabangu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye atazichapa na Hussein Itaba wa Tanzania atawasili Jumanne usiku huku mpinzani wa bondia Zulfa Macho wa Tanzania, Alice Mbewe akitarajiwa kuwasili mapema.

Twissa amesema, kila kitu kiko katika hatua za mwisho na tiketi zitaanza kuuzwa kwa njia ya Nilipe na Selcom kwa shilingi milioni tatu kwa meza ya watu 10 na shilingi 150,000  kwa viti vya kawaida.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news