Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na operesheni kali ya kukamata watu wanaofanya mipango ya kuhamasisha maandamano bila kufuata sheria na kusababisha taharuki kwa wananchi sambamba na mipango ya kuharibu mali, miundombinu na kudhuru watu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,SACP Lazaro Mambosasa leo Novemba 3,2020.
"Hadi sasa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watu 14 kama ifuatavyo; Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Boniface Jacob aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo na mwanachama wa Chadema, Denis Vesta, Godfrey Seleman, Elisha Mbandamka, Shehebu Kiarus na Yohana Marco.
"Wengine ni Salehe Omary, Mohamed Omary, Tundu Antipas Lissu aliyekuwa mgombea Urais na Makamu Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Moses Fanuel Omary, Charles Renatus, Essau Charles Bwiru, na Godbless Lema aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Arusha Mjini,"amesema Kamanda Mambosasa.
Amesema, watuhumiwa wote wamekamatwa katika maeneo mbalimbali na upelelezi unaendelea na watuhumiwa watatu akiwemo Tundu Lissu wameachiliwa kwa dhamana ya Polisi na jalada limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi za kisheria.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Mambosasa amesema, Jiji la Dar es Salaam liko shwari na wanasiasa waache tabia ya kuja kufanya fujo maeneo ambayo sio majimbo yao na hatimaye wafuate sheria ili kupeleka malalamiko yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi na si kushawishi watu kufanya maandamano haramu, kuhatarisha maisha ya watu na mali zao pia kuleta taharuki kwa wananchi wasio na hatia.
"Aidha, watuhumiwa wengine wanaotafutwa ni pamoja na Halima Mdee ambaye alikuwa mgombea Ubunge Jimbo la Kawe kupitia Chama cha CHADEMA pamoja na Zitto Zuberi Kabwe ambaye ni kiongozi mkuu wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT wazalendo) aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini,"amesema Kamanda Mambosasa.
Pia amesema, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawataka wajisalimishe mara moja ili kuendelea na mahojiano kwa tuhuma zinazowakabili.
Tags
Habari