PROF.MCHEMBE AWAAGIZA WATAALAMU WA SEKTA YA AFYA KUFIKIRIA HUDUMA BORA NA NAFUU KWA WANANCHI

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe ametoa wito kwa Wataalamu wa Sekta ya Afya nchini kuhakikisha wanafikiria namna ya utoaji huduma bora na kwa gharama nafuu ili wananchi wenye hali zote waweze kuzimudu.
Wito huo ameutoa leo, wakati akifungua Mkutano wa saba wa Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Watumishi kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau mbali mbali wanaojihusisha na masuala ya afya nchini.

"Ni wajibu wetu sisi, tukiwa kwenye Mkutano huu wa wa Afya kuwaza vyema tunamsaidiaje mwananchi wa hali ya chini kupata huduma bora, zenye unafuu na zinazofikika kila sehemu bila kumuumiza mwananchi," amesema Prof. Mchembe.

Hata hivyo, Prof. Mchembe amesema kuwa, Wizara ya Afya itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote ili kufanikisha utoaji huduma bora na nafuu kwa wananchi, huku akiweka wazi kuwa kama Serikali itatendea kazi mapendekezo na ushauri utakaotokana na Mkutano huo. 

Aidha, Prof. Mchembe amesisitiza kuwa, ni muhimu mijadala itayoendelea katika mkutano huo kuhakikisha inapita kwenye malengo ya Wizara yakiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto, kupunguza maambukizi ya VVU, TB, Ukoma.

Mbali na hayo, Prof. Mabula Mchembe amewataka Wataalamu hao kujadili masuala ya kupunguza magonjwa yasiyo yakuambukiza ambayo yanaongeza mzigo kwa Serikali kutokana na gharama za kuyatibu magonjwa hayo, yanayotokana na mtindo wa maisha ikiwemo matumizi ya pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi.Naye, Mkurugenzi Idara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa, Serikali imefanya maboresho mengi sana katika miaka saba iliyopita, huku akiweka wazi kuwa mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho yataendana na mpango mkakati wa Sekta afya unaosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya. 

Pia, Dkt.Kapologwe amesema kuwa, kama wasimamizi wa Sera watahakikisha maazimio yatakayotoka kwenye kikao hicho yanaingizwa kwenye mipango ya utekelezaji kwenye Hospitali zote ngazi ya Wilaya, Halmashauri na zahanati kwa utekelezaji zaidi. 

"Katika kikao hiki, pamoja na maelekezo ambayo utayatoa, sisi tukiwa kama wasaidizi wako tutahakikisha, maelekezo yako pamoja na maazimio utakayotoa katika kikao hiki, tunaenda kuyaingiza katika mipango yetu katika Hospitali za Mikoa, Halmashauri na Zahanati,"amesema Dkt. Ntuli Kapologwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news