Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametembelea Bandari ya Malindi jijini Zanzibar pamoja na eneo la Maruhubi kwa ajili ya kutafuta mwarobaini wa ucheleweleshwaji wa kutolewa kwa mizigo bandarini hapo.
Ziara hiyo ya Dkt. Husein Mwinyi ni ya kwanza kuifanya mara tu baada ya kushika wadhifa wa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambapo alifika bandarini hapo kujua sababu zinazopelekea kuchelewa kushushwa kwa mizigo, mrundikano wa makontena pamoja na meli kukaa kwa muda mrefu nje ya bandari hiyo.
Katika maelezo yake, Dkt. Hussein Mwinyi amesisitiza kufanyika jitihada za makusudi za kutafuta ufumbuzi wa kuondoa makontena bandarini hapo kwa lengo la kuondosha usumbufu na mrundikano wa makontena katika eneo hilo.
Rais Mwinyi amesema kuwa, uchumi wa Zanzibar unategemea sana bandari na pale pasipokuwepo ufanisi katika utendaji wa shughuli zake ni dhahiri kwamba uchumi hauwezi kuimarika.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Bandari, Ali Haji Haji wakati alipofanya ziara ya hafla kutembelea Bandari ya Malindi Novemba 3,2020.
Ameongeza kwamba, katika hali ya sasa kuna meli zinateremsha mizigo katika bandari za Mombasa na Dar es Salaam na hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara kiasi ambacho huwasababishia kupata hasara.
Amesema kuwa, wapo baadhi ya wafanyabiashara walioamua kutokuleta mizigo yao Zanzibar kutokana na mizigo yao kukaa kwa muda mrefu, hivyo amesisitiza haja ya kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto hiyo.
Rais Dky. Husein ameutaka uongozi huo wa bandari kuongeza kasi ya ushushaji wa mizingo ili kupunguza muda wa kukaa meli muda mrefu nje ya bandari.
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kumekuwepo changamoto ya kupanda bei kwa bidhaa kiholela kutokana na utendaji wa bandari.
Amesisitiza haja ya kuwepo kwa eneo la kuweka makontena (bandari kavu) ili kuondosha mrundikano wa makontena katika eneo hilo la bandari ya Malindi.
Hivyo, Rais Dkt. Hussein ameusisitiza uongozi huo kuona haja ya kuwajibika kwa kufahamu kuwa bandari ni kitovu cha uchumi wa nchi huku akizuia utumiaji wa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya upembuzi yakinifu katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kuweka makontena (bandari kavu) huko Maruhubi.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameutaka uongozi huo kutumia fedha walizonazo ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za bandari.
Akitoa maelezo Mkurugenzi Mwendeshaji Juma Sururu Juma amesema kuwa, miongoni mwa sababu za zinazosababisha kuwepo mrundikano wa makontena bandarini hapo ni kuchelewa kwa baadhi ya wafanyabiashara kutoa mizigo yao pamoja na masuala mengine ya kiofisi.
Aidha, Mkurugenzi huyo alieleza shughuli za bandari hiyo ya Malindi huku akieleza kuwa mizigo ambayo haichelewi kutolewa bandarini hapo ni pamoja na ile ya vyakula, saruji na mafuta hizo ni bidhaa zinazoletwa na wafanyabishara maalum.
Akieleza kuhusu ukaaji wa meli Bandarini hapo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa meli haikai zaidi ya siku tano na tayari inakuwa imeshaondoka hasa ikizingatiwa kwamba shughuli hizo zinafanywa usiku na mchana.
Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Ali Haji Haji alieleza kuwa katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo lilipatikana eneo la Maruhubi kwa ajili ya eneo la makontena (bandari kavu) na ndilo wanalokusudia kulifanyia shughuli hizo.
Viongozi hao katika maelezo yao walieleza kuwa msongamano wa makontena ndio sababu inayopelekea ufinyu wa nafasi katika eneo hilo la bandari ya Malindi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Kaimu Mkurugenzi Huduma za bandari, Juma Sururu Juma wakifuatana pamoja na Ujumbe wake wakati alipotembelea Bandari ya Malindi jijini Zanzibar.
Kaimu huyo Mkurugenzi alimueleza Rais Dkt. Hussein kuwa pindi itakapopatikana nafasi wataweza kutumia zamu tatu za kufanya kazi kwa siku na hivyo, kuondokana na tatizo la meli kukaa nje ya bandarini muda mrefu.
Pamoja na hayo, viongozi hao walieleza kuwa njia moja wapo ya kutatua tatizo hilo na kupata mwarobaini wake ni kuanzisha eneo la kuwekea makontena (bandari kavu) ambalo katika mitizamo yao waligundua eneo hilo la Maruhubi.
Rais Dkt. Hussein ametembelea eneo hilo la Maruhubi lililotengwa na Shirika hilo la Bandari kwa ajili ya kuweka makontena (bandari kavu) huku Kaimu Mkurugenzi huyo akieleza kuwa ni vyema bandari hiyo ikawa karibu na bandari kuu ili kupunguza gharama na kubainisha kuwa kazi zote za kupeleka na kuondoa makontena matupu zitafanyika wakati wa usiku.