Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hafla hiyo ya kiapo imefanyika leo Novemba 9, 2020 Ikulu jijini Zanzibar ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othamn Mkungu, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Hassan Khatib Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, Naibu Mufti Mkuu Sheikh Mussa Wadi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Hassan Khatib Hassan, Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Juma Kinana, wakuu wa vikosi vya Ulinzi na Usalama, viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wanafamilia.
Akizungumza mara baada ya kiapo hicho, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kumuamini na kumteua kuwa Msaidizi wake namba moja na kuahidi kwamba atamsaidia kwa asilimia mia moja.
Ameeleza kwamba, uteuzi huo ameupokea vizuri na kwa sababu Rais kamteua akiamini kwamba anaweza kumsaidia hivyo, aliwaahidi wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla kwamba atafanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na kuhakikisha yale malengo ya Serikali yaliyowekwa yanafikiwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema kwamba, katika hilo yapo mambo ambayo yatajitokeza hapo baadae ambapo watatokea baadhi ya watu ambao watakuwa hawako tayari kuyatekeleza hivyo, alisema kwamba akiwa Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali hatokuwa na muhali wa aina yoyote na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa ili kuweza kupata watu watakaoendana na kasi ya Mhe. Rais.
Amesema kwamba, wananchi wanamategemeo makubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hasa baada ya Rais wa Zanzibar kushinda uchaguzi mkuu kwa kishindo kikubwa.
Ameongeza kwamba, malengo ndani ya Serikali ni kuhakikisha matumaini yanarejeshwa kama vile Rais alivyoahidi kuyatekeleza katika kampeni zake kipindi ambacho anaomba fursa ya kuchaguliwa kuwa Rais.
Aidha, amesema kwamba atasimamia na kumsaidia Rais kwa asilimia mia na atatumia nguvu zake zote na hekima na busara zake zote katika kuhakikisha malengo hayo yanatimia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliteuliwa jana Novemba 8,2020 na Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Kifungu Namba 39 (1) na 39 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ni miongoni mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walioteuliwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi mnamo tarehe 07 Novemba 2020 kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Kifungu Namba 66 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Kabla ya uteuzi huo, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba.